Waziri ataka mazingira bora uwekezaji SADC

06Aug 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri ataka mazingira bora uwekezaji SADC

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ametoa wito kwa nchi zote za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kutilia mkazo uboreshaji wa mazingira wezeshi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika viwanda.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Alitoa rai hiyo jana wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC jijini Dar es Salaam, akiungwa mkono na Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Dk. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte.

Watatu hao pia walimpongeza Rais John Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda nchini.Bashungwa alisema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika biashara ndani ya SADC katika mauzo.

Alibainisha kuwa mauzo ya Tanzania kwenda nchi za SADC kwa mwaka 2018 yalikuwa Dola za Marekani milioni 999 ikilinganishwa na Dola milioni 875 mwaka 2017.

Alisemu takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la asilimia 12.16 na uingizaji wa bidhaa Tanzania kutoka SADC uliongezeka kutoka Dola milioni 600.64 mwaka 2017 hadi kufikia Dola milioni 604.32 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.61.

Alitaja bidhaa muhimu ambazo Tanzania inauza SADC kuwa ni pamoja na madini mbalimbali kama vile tanzanite na dhahabu, bidhaa za kilimo kama vile chai na kahawa, bidhaa za viwandani kama vile plastiki, tumbaku, saruji, marumaru, dawa na vifaa tiba.

Alisema bidhaa ambazo Tanzania inanunua kwa wingi kutoka nchi za SADC zinahusisha magari, mbegu za mahindi, gesi, mabati, vilainishi, bia na sukari.

Alisema bidhaa hizo zaidi zinatoka katika nchi za Afrika Kusini, Zambia, Mauritius na Malawi.  

Alisema Tanzania pia inanufaika na miradi mbalimbali ya ushirikiano inayotekelezwa katika nchi za SADC hususan miradi inayounganisha nchi jirani.

Aliitaja kuwa ni pamoja na mradi wa vituo vya pamoja vya forodha vya mpakani kati ya Tanzania na Zambia (Tunduma) na kati ya Tanzania na Malawi (Nakonde) na mradi wa maendeleo ya maji na uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe.

Waziri wa Viwanda na Biashara Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Amina Ally, alisema serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanya kazi kubwa kuwaletea maendeleo wananchi, hasa katika kuimarisha miundombinu.

“Tunakupongeza Rais Magufuli kwa uthubutu wa kuendeleza kile kilichoanzishwa na Mwalimu Nyerere kwa kuendeleza bwawa la kufua umeme kwa manufaa ya Watanzania na nje ya Tanzania,” alisema.

Katibu Mtendaji wa SADC (Dk. Taxe) alisema uendelezaji wa viwanda unahitaji mambo mengi ikiwamo umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

“Huwezi kuwa na viwanda kama huna umeme unaozalisha kwa urahisi na unafuu, kuwa na umeme unaotakiwa ni kitu cha muhimu sana, pongezi kwa Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa umeme na kuendelea na mradi wa Mto Rufiji,” alisema.

Kiongozi huyo wa SADC aliwataka Watanzania kutumia fursa zilizoko kwenye soko la SADC linalojumuisha nchi 16, zenye watu wapatao milioni 344.

Mwenyekiti wa Baraza la Biashara wa SADC, Charity Mwiya kutoka Namibia, alisema wanawake wanapaswa kujengewa mazingira wezeshi ili kupata fursa ikiwamo kufanya biashara.

"Nimeangalia katika orodha ya watoa mada wengi ni wanaume, ila natambua kwamba wengi wao wapo huko kwenye mabanda wakionyesha bidhaa mbalimbali, mimi ni mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa kamati hii, naelewa hali ilivyo,” alisema.