Waziri ataka utatuzi kero upatikanaji dawa

23Jan 2022
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waziri ataka utatuzi kero upatikanaji dawa

​​​​​​​WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kutatua kero ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, kutoka asilimia 50 ya sasa hadi kufikia asilimia 90, ndani ya miezi mitatu.

Waziri Ummy alitoa agizo hilo jana mkoani Dar es Salaam, alipotembelea MSD na kuzungumza na menejimenti kuhusu changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.

Alisema amepata changamoto hizo kutoka kwa baadhi ya vituo vya afya na wananchi aliokutana nao na kwamba lazima itatuliwe haraka iwezekanavyo, huku akisisitiza upatikanaji wa dawa muhimu ambazo wananchi wanaandikiwa na daktari.

“Hakikisheni upatikanaji wa dawa muhimu zote katika vituo vya kutolea huduma za afya. Rais Samia Suluhu Hassan alituwezesha kupata fedha za kununua dawa, hivyo hakuna sababu ya ukosefu wa dawa na hili nitalisimamia kikamilifu kuhakikisha dawa zinanunuliwa na kusambazwa kwenye vituo kwa wakati,” alisema Waziri Ummy.

Pia waziri huyo ametembelea maghala ya kuhifadhia dawa ya MSD, sambamba na kujionea vifaa mbalimbali vya maabara pamoja na vitendanishi vyake.

Katika hatua nyingine, Ummy alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD na timu yake kwa kufanya vizuri katika kusimamia uanzishaji wa viwanda vya ndani vya dawa.

Aliwataka kuendelea kubuni zaidi aina ya viwanda vitakavyozalisha bidhaa muhimu za afya ili kutatua changamoto za dawa na vifaa tiba nchini.

Pia alielezea kufurahishwa na juhudi za MSD za kuwezesha upatikanaji wa mashine za kusafisha damu kwa bei nafuu ambazo zitapunguza gharama kwa zaidi ya asilimia 50.

Habari Kubwa