Waziri atamani sera ya ugatuzi wa madaraka

14May 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Waziri atamani sera ya ugatuzi wa madaraka

WAZIRI wa Nchi, ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa, Selemani Jafo, amesema kuwa kutokuwapo kwa sera ya ugatuaji madaraka iliyojengwa kwenye mfumo wa kisheria ni moja ya changamoto iliyosababisha Serikali kufanya mapitio.

WAZIRI wa Nchi, ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa, Selemani Jafo,.

Jafo aliyabainisha hayo jana alipokuwa akifungua kikao kazi kilichokutanisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kutoka mikoa yote 26 kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo kwenye rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka.

Alisema changamoto moja wapo ni kutokuwapo kwa sera ya ugatuaji iliyojengwa kwenye mfumo wa kisheria inayoelekeza mipaka, majukumu na utaratibu wa utekelezaji wake, jambo ambalo linafanya ionekane kama ni hiari na utashi.

Aidha Jafo alisema changamoto nyingine ni kuwapo kwa mitazamo inayokinzana kati ya watendaji na viongozi wa kisiasa katika ngazi ya vijiji, kata na halmashauri katika kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alisema pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikitegemea fedha kwa kiasi kikubwa kutoka Serikali kuu na kutolea mfano kwa mwaka 2018 zilitegemea zaidi ya asilimia 88 ya mapato.

Jafo amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo hayo ili kuboresha rasimu hiyo kwa maslahi mapana ya wananchi, wadau na taifa kwa ujumla.

Jafo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa ukabilifu fedha na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za wilaya, ujenzi wa mabweni, madarasa, vyoo katika shule za msingi na sekondari ambayo tayari fedha zake zimeshatolewa na serikali.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, aliahidi ushiriki mzuri wa wa wakuu hao kwa kuwa wao ndio wanaotoka kwa wananchi.

Pia alimwakikishia Waziri Jafo kuwa watasimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwa itakamilika katika muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.

Mwakilishi wa UNICEF, Pius Chaya, alisema ajenda ya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka imekuja wakati mwafaka, kwa sababu serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma wanazostahili na ambazo zinawafikia kwa wakati.

Aidha, Chaya alisema wadau wa maendeo ambao pia wameshiriki katika machakato wa mapitio ya sera hiyo wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Habari Kubwa