Waziri atishia kuvunja mkataba na kiwanda

22May 2019
Frank Monyo
DAR
Nipashe
Waziri atishia kuvunja mkataba na kiwanda

WAZIRI wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, ametishia kuvunja mkataba na kiwanda cha kutengeneza mabomba cha Tanzania Steel Pipe (TSP) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam baada ya kushindwa kupeleka kwa wakati mabomba kwa ajili ya miradi ya maji -

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akitoa maagizo kwa Meneja Biashara wa Kiwanda cha Tanzania Steel Pipe (TSP), Ryan Koh (kushoto) alipofika kiwandani hapo.

katika kijiji cha Nyang'hwale-Geita na Longido mkoani Arusha.

 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya  kufanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho jana, kufahamu tatizo linalosababisha mabomba hayo kushindwa kufika kwenye maeneo ya kazi  kwa wakati na kusababisha utekelezaji wa miradi hiyo kusuasua bila sababu za msingi."Nategemea kuona Kiwanda cha Tanzania Steel Pipe kinaheshimu mkataba tuliongia nao wa kupeleka mabomba ya maji kwa ajili ya kazi za ujenzi wa miradi ya Nyang'hwale-Geita na Longido-Arusha iweze kukamilika....Kinyume cha hapo sitakuwa tayari kuona miradi hiyo ikishindwa kukamilika kwa wakati na wananchi kukosa maji, niko tayari kutafuta kampuni nyingine itakayofanya kazi yetu kwa uaminifu,” alisema Prof. Mbarawa na kuongeza:

"Nimekuwa nikikerwa na tabia ya makandarasi kushindwa kukamilisha miradi ya Nyang'hwale na Longido kwa sababu ya upatikanaji wa mabomba si mzuri bila kuwapo  sababu zozote za msingi kufika… kwangu kiwandani hapa ni kutaka kufahamu kuna tatizo gani kwa kuwa ndio wenye mkataba wa kupeleka mabomba kwenye miradi hiyo.”Prof. Mbarawa alikutana na Meneja Biashara wa TSP, Ryan Koh, na kumuonya kuwa endapo wataendelea kutoheshimu mkataba huo na kuendelea kuwa sababu ya miradi hiyo kuchelewa, hatasita kusitisha mkataba huo na kutafuta kampuni nyingine.Waziri Mbarawa alisisitiza kuwa hatoweza kuvumilia ucheleweshwaji wa mabomba hayo, huku wananchi wa maeneo hayo wakiendelea kuteseka."Nimeongea na Mkurugenzi wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira wizarani, ahakikishe kama kuna madeni yoyote mnayodai awalipe kufikia Jumatano (leo),” alisema Mbarawa.

Kwa upande wake, Koh alisema amepokea ujumbe huo na wataanza kupeleka mabomba hayo mara moja katika maeneo ya kazi ya miradi hiyo na kumshukuru Prof. Mbarawa kwa kufika kiwandani kusikiliza changamoto zao.Miradi ya Maji ya Nyang'hwale na Longido ni moja ya miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa lengo la kufikisha huduma hiyo muhimu kwa kila mwananchi.

Habari Kubwa