Waziri atoa miezi mitano ujenzi soko

27Jan 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri atoa miezi mitano ujenzi soko

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amekerwa na kukithiri kwa uchafu katika Soko la Sabasaba jijini Dodoma, huku akiagiza ujenzi kuanza kabla ya Juni mwaka huu.

Agizo hilo alilitoa jana jijini hapa baada ya kutembelea soko hilo kujionea hali ya uchafu.

Katika ziara hiyo, Jafo alijionea mifereji ya maji ya mvua ikiwa imejaa uchafu, jambo ambalo linahatarisha afya za wafanyabiashara wa eneo hilo.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo, waziri huyo alisema hakutarajia kushuhudia soko la aina hiyo linalohatarisha afya za watu kwenye jiji linalokusanya mapato zaidi ya Sh. bilioni 71.

"Nataka Soko la Sabasaba kabla ya mwaka wa fedha kuisha, ujenzi uanze kwenye soko hili, mrekebishe mazingira ya wafanyabiashara, haiwezekani mkusanye zaidi ya Sh. bilioni 71 halafu mkaliacha hili soko hivi," alionya.

Jafo pia aliutaka uongozi wa jiji hilo kuachana na ujenzi wa hoteli ya nyota tatu ili uboreshe kwanza mazingira ya wafanyabiashara wa soko hilo.

Aliutaka uongozi huo kuhakikisha unasimamia usafi ili kulinda afya na usalama wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkufya Msekeni, alisema tayari jiji limeshaandaa mchoro kwa ajili ya kujenga soko hilo.

Awali, mfanyabiashara aliyekutwa na waziri sokoni hapo, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakizungumzia suala la uchafu katika soko hilo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

"Hili soko wafanyabiashara wa Majengo na Chang'ombe wanakuja kuchukua bidhaa, lakini limetelekezwa, halifanyiwi usafi, mifereji ya kupitishia maji hakuna, mazingira kwa ujumla ni machafu, kipindupindu hapa kipo nje nje, Waziri tunaomba utusaidie," alisema.

Habari Kubwa