Waziri atoa tamko wajawazito kulazwa kwenye meza kliniki

23Jan 2021
Dinna Stephano
Tarime
Nipashe
Waziri atoa tamko wajawazito kulazwa kwenye meza kliniki

SIKU moja baada ya Nipashe kuripoti kuhusu watoto kupimwa uzito chini ya mti na wajawazito kupimiwa juu ya meza, kutokana na kukosa huduma ya zahanati kijijini Nyagisya, Kata ya Kiore wilayani Tarime mkoani Mara, wataalamu wa afya wamefika katika kijiji hicho kuchukua hatua.

Vilevile, serikali kupitia wizara yenye dhamana ya afya, imetoa tamko kuhusu suala hilo, akiahidi kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Baada ya kufika kijijini huko jana, wataalamu hao walipiga marufuku upimaji huo uliokuwa ukifanyika chini ya mti na kuagiza chumba kimoja cha ofisi ya kijiji kufanyiwa ukarabati, ili kitumike kutoa huduma za afya.

Viongozi waliofika kijijini huko jana ni pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sylvanus Gwiboha, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Amos Manya, Daktari Joshua Karaba kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu na Mhandisi Ujenzi, Ernest Maungo.

Wengine ni Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kata ya Mtana, Seif Athuman, pamoja na Leonard Nyakanga ambaye ni Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini.

Viongozi hao walifanya kikao na uongozi wa serikali ya kijiji na Diwani wa Kiore, Rhobi John, kujadili juu ya huduma ya kliniki inayotolewa chini ya mti na wajawazito kupimwa juu ya meza.

Baada ya kikao hicho, wataalamu hao waliwahoji wananchi ili kupata ukweli wa yale yaliyoripotiwa na Nipashe, kisha wakatembelea ujenzi wa zahanati kwa ajili ya kijiji hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Gwiboha, alisema wamepiga marufuku huduma kutolewa chini ya mti kwa kuwa ni kinyume cha mwongozo wa serikali.

Alisema huduma hiyo inatakiwa kutolewa kwenye majengo ya serikali au binafsi kulingana na maandalizi ya kijiji husika.
"Ni jambo zuri kusogeza huduma ya afya karibu na wananchi maana inawasaidia kupunguza umbali, lakini siyo kutoa huduma chini ya mti, isipokuwa kwenye majengo ya serikali na binafsi.

"Kama ofisi ya kijiji kulikuwa na kikao, walipaswa kuahirisha kikao ili huduma ya kliniki iendelee.

"Ukaguzi wetu ulianzia kwenye Zahanati ya Mtana, nikamuuliza Muuguzi Rebeka Samson kwanini anatoa huduma chini ya mti, akasema ofisi ya kijiji walikuwa na kikao, nikamwambia nimekuona kwenye picha gazeti la Nipashe umependeza kweli, lakini mbona hukuvaa sare za kazi? Hilo ni kosa.

"Nikamuuliza mtendaji wa kijiji, akasema yeye amehamishiwa hapo ana miezi minne na kwamba kuna chumba cha kliniki ila kimejaa mchwa na kuna wakati waliona hadi nyoka wakaona siyo salama," alisema Gwiboha.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa halmashauri itafanya ukarabati wa chumba hicho na huduma ya kliniki itaendelea kutolewa katika kijiji hicho katika ofisi ya serikali ya kijiji na hatua za ukarabati zinaendelea, akiahidi kutoa mifuko saba ya saruji.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyagisya ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Central, Ghati John, alikiri maofisa hao kufika kwenye kijiji chao na walifanya kikao na kuzungumza na wananchi na kisha kutembelea eneo panapojengwa zahanati.

"Walikuja kuthibitisha kama yanayofanyika ni kweli na wakahoji wananchi, wakawaeleza ukweli ndivyo ilivyo, wao walidhani picha ni za kutengeneza, lakini wameelezwa kila kitu, bahati nzuri alikuwapo mwananchi ambaye ndiye alinunua godoro la wajawazito kulalia wakati wa kliniki.

"Tukawaonyesha chumba tulichotengwa, lakini kimejaa mchwa, mmoja akatoa Sh. 10,000, kwa ajili ya kuweka kibarua afanye usafi," alisema John.

KAULI YA WIZARA

Jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alitoa taarifa kuhusu utolewaji wa huduma za afya kwa watoto na wajawazito kijijini Nyagisya chini ya mti na ndani ya darasa.

Katika taarifa yake hiyo, waziri huyo alisema katika gazeti la Nipashe ameona picha za watoto wakipimwa uzito chini ya mti.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali iliwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu ya kutolea huduma za afya hasa huduma ya afya ya msingi na sekta ya afya kwa ujumla wake.

"Serikali imesikitishwa na hali hiyo, hivyo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, inafuatiliaji kwa karibu kujua nini kilitokea hadi kufikia hatua hiyo.

"Badala ya kutumia majengo mengine ya serikali yaliyopo katika eneo la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na hatua zitachukuliwa baada ya kupata maelezo ya kina kujua nini kilitokea," alisema Dk. Gwajima katika taarifa yake ya jana.

Habari Kubwa