Waziri awafunda wahitimu maliasili

15Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Katavi
Nipashe
Waziri awafunda wahitimu maliasili

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, amewataka askari wa misitu waliohitimu mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanarejesha uoto wake wa asili katika maeneo yote ya misitu ambayo yameharibiwa.

Kanyasu alisema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa askari 140 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani Katavi.

“Leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli wa TFS, lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mazingira, na hatuwezi kusema zisiendelee. Zinatakiwa kuendelea katika namna ambayo haitaifanya nchi yetu kuwa jangwa.

“Kuhitimu kwenu hakumaanisha mnakwenda kuzuia maendeleo, kunamaanisha mnakwenda kushirikiana na wanaotaka maendeleo kwa kufanya kazi wakifikiria maendeleo endelevu,” alisema.

Alisema kwa sasa  nchi inakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabinchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira ikiwamo ukataji wa miti, ukame, mvua nyingi na mafuriko ambapo vyote hivyo husababishwa na matumizi mabaya ya kazi za kiuchumi.

Kanyasu alisema ni matarajio ya serikali baada ya askari hao kuhitimu pamoja na kazi yao ya msingi ya ulinzi watafanya kazi ya kuhakikisha wanarejesha uoto wa asili uliopotea.

Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisema taifa limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuhifadhi ikiwamo shughuli za kibinadamu pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa watumishi na mambo yote hayo yanapelekea mafunzo hayo kuwa muhimu katika uhifadhi wa mapori na misitu ya hifadhi nchini.

Habari Kubwa