Waziri awajibu kina Nape ukusanyaji kodi kwa mtutu

14Feb 2021
Godfrey Mushi
Dodoma
Nipashe Jumapili
Waziri awajibu kina Nape ukusanyaji kodi kwa mtutu

SERIKALI imetetea uamuzi wake wa kutumia vikosi kazi ‘task force’ katika kukusanya kodi kwa wafanyabiashara na walipa kodi wakubwa wanaokwepa kodi, ikifafanua kuwa kabla ya kutumia kikosi, hutumwa kwanza timu maalum kwenda kukagua ikiwahusisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wataalamu wengine.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema serikali hufanya hivyo panapotokea watu wanafanya njama za kukwepa kodi, ndipo Kamishna Mkuu wa TRA, hutumia sheria inayomruhusu kutengeneza kikosi kazi kwa mujibu wa Sura ya 348 ya Sheria ya Utawala wa Kodi.

Dk. Mwigulu alitoa ufafanuzi huo jana bungeni alipokuwa anajibu hoja za wabunge waliohoji uhalali wa matumizi ya kikosi kazi kukusanya kodi.

Hoja hiyo iliibuliwa bungeni Februari 9, mwaka huu na Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, akidai ukusanyaji wa kodi kupitia vikosi kazi unaua biashara na kushauri kazi hiyo ifanywe na wenye taaluma chini ya TRA.

Pia, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu, alisisitiza ni lazima Wizara ya Fedha na Mipango iwasikilize wananchi kwa sababu inawezekana hawana taarifa sahihi, hivyo biashara zinakufa.

Katika hotuba ya kuhitimisha mjadala huo jana aliyoitoa kwa niaba ya Waziri na Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri Mwingulu alisema:

"Tuna kipindi tumekipita ambacho kulipa kodi, elimu ya mlipakodi, uhiari na uzalendo ilikuwa jambo kubwa na gumu sana kwa watu watu walio wengi, hasahasa wafanyabiashara wakubwa.

"Nendeni mkafuatilie 'hansad' (taarifa) za Bunge lile lililopita, fuatilieni hansad muone kilio kikubwa kilikuwa wapi.

“Kilio kikubwa kilikuwa walipakodi hasa wakubwa, hawalipi kodi ipasavyo. Walipakodi waliokuwa wanabeba nchi, ni watumishi wa umma kwa kiwango kikubwa, na walipakodi wadogo wadogo na baadhi yao walipakodi wakubwa waliokuwa waaminifu. Kwa hiyo kuna kiwango kikubwa sana cha ukwepaji wa kodi.

"Sasa, hivi jambo linaloanza kujitokeza la kwamba task force ndio zinakusanya na TRA imeacha majukumu yake, ninaomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba TRA bado wanaendelea kukusanya mapato wao wenyewe, na pale ambapo inatokea task force inakusanya, kunakuwapo hatua zinazofuatwa.

“Kunakuwapo na taarifa kwamba kwa mlipakodi huyu kuna viashiria vya kutokulipa kodi ipasavyo. Baada ya hapo, kunatumwa timu ya kwenda kukagua, timu ya kawaida ambayo ni TRA na wataalamu wao huenda kukagua. Wakishakagua wanaambizana, wanaelekezana kwa mujibu wa sheria."

Waziri huyo alisema kuwa kabla ya kikosi kazi kwenda kufanya kazi yake, TRA kwa kutumia sheria zake, hujadiliana na mlipakodi katika yale makadirio, wanakubaliana na wakati mwingine wanatiliana saini.

Habari Kubwa