Waziri awaonya 'trafiki' waviziaji

24Apr 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Waziri awaonya 'trafiki' waviziaji

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, amewataka askari wa usalama barabarani wenye tabia ya kukamata daladala ovyo kwa kujificha chini ya mwamvuli wa Sheria ya Usalama Barabarani, waache mara moja.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni.

Masauni alitoa onyo hilo jana bungeni jijini Dodoma alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Rose Tweve (CCM), aliyedai kumekuwa na changamoto ya askari hao kusimamisha daladala ovyo ili kukagua kama kondakta na dereva wamevaa sare wakati jambo hilo linatakiwa kufanyika kabla gari kuanza safari, hivyo kusababisha wananchi kuchelewa kuripoti kazini.

Masauni alisema sheria hiyo iliyorejewa mwaka 2002 inampa mamlaka askari kupitia kifungu cha 81 kusimamisha gari lolote barabarani au sehemu yoyote anapolitilia shaka na kulikagua au pindi linapokuwa limetenda kosa.

“Kuwa na utaratibu wa lazima, kama serikali tumeshalitafakari kwa kina na haliepukiki katika karne hii kwa kuwa tunahitaji kuwa na magari salama," alisema.

Aliongeza kuwa katika mabadiliko ya sheria yanayokuja, suala hilo litasimamiwa na baraza jipya la usalama barabarani.

“Jeshi la Polisi limeshaandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi vya mabasi ya umma na tunataka utaratibu huu uanze haraka,” alisema.

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alihoji ni lini serikali itaandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi ili kusaidia matumizi mazuri ya muda kwa magari yanayobeba abiria hususan daladala.

Masauni alisema ukaguzi wa pembezoni mwa barabara ambao huhusisha mabasi ya daladala na vyombo vingine vya moto, hufanyika katika vituo vya ukaguzi maalum ambavyo vipo katika barabara kuu na vingine vya miji na majiji.

Alisema uwapo wa ukaguzi ni jambo la msingi ili kuongeza mapato kwa Jeshi la Polisi na kwamba mabadiliko yajayo ya sheria yatasimamiwa na baraza jipya la usalama barabarani litakalokuwa na muundo mpya.

Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige (CCM), alihoji ni lini stahiki za askari wanaopata ajali wakiwa kazini zitalipwa.

Katika majibu yake kwa mbunge huyo, Masauni alikiri kuwapo kwa changamoto nyingi kwenye malipo ya askari nchi nzima, lakini kwa sasa sehemu kubwa ya malimbikizo yameanza kulipwa.

"Malipo yaliyobaki yatakamilishwa kuendana na uhakiki na upatikanaji wa fedha zitakazotengwa kwa ajili ya zoezi hilo,” Masauni alisema.

 

Habari Kubwa