Waziri azitaka halmashauri kujifunza Ikungi

12Dec 2019
Juster Prudence
Singida
Nipashe
Waziri azitaka halmashauri kujifunza Ikungi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amezitaka halmashauri nchini kwenda kujifunza Ikungi, mkoani Singida ambao wamejenga majengo kwa viwango na kwa fedha kidogo iliyotolewa na serikali.

Selemani Jafo

“Nilidhani mnaigiza kwamba mmesikia waziri anakuja mkaanza kujenga ila ninaona hapa ujenzi unaendelea vizuri, nawapongeza sana Mzinga, jukumu letu ni kutafuta kazi, tunataka jengo likamilike wananchi wapate huduma, wafanyekazi kwenye ofisi na siyo madarasa,” alisema.

Aidha, alisema Halmashauri ya Ikungi ni ya kuigwa kwa kuwa wametumia Sh. bilioni 1.5 kujenga ukumbi na ofisi za watumishi, na kwamba wapo wanaong’ang’ani kujenga ghorofa na kutumia fedha nyingi.

“Unakuta Mkurugenzi anang’ang’ania kujenga ghorofa ametumia bilioni mbili au sita halafu watumishi bado wanakaa kwenye vichaka, hapa Sh. bilioni 1.4 mmepata ofisi safi na watumishi wanakaa pazuri. Watu waje kujifunza Ikungi kwenye matumizi ya fedha za umma,” alisema Jafo na kuongeza:

“Nikusifu sana mkurugenzi na ofisi yako ni nzuri na safi sana, nimeenda Wanging’ombe nimekuta ofisi imegeuzwa karakana, mipira imejaa ndani, uchafu tuu, hapa ofisi mtu akifika safi inapendeza:

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Ikungi, Justice Kijazi, alisema ukumbi wa halmashauri limejengwa jengo kwa Sh. milioni 420 na kuweka samani ndani, na kwamba kwa sasa vikao vya halmashauri vinafanyika humo ikiwamo kukodisha kwa ajili ya sherehe mbalimbali.

Wakati huo huo, akiwa wilaya ya Iramba, alieleza kuchukizwa na wizi wa vifaa ya ujenzi unaoendelea na kwamba limekuwa jambo la kujirudia mara kwa mara licha ya kwamba aliwahi kukataza jambo hilo kabla na kuongeza kuwa vifaa vinavyoibiwa ndivyo vinavyotegemewa katika ujenzi wa miradi mbalimbali.

Jafo aliwataka Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba kutoa maelezo juu ya tukio hilo ifikapo Ijumaa ya Desemba 13, mwaka huu.

Habari Kubwa