Waziri azuia ‘malipo ya corona’ shule binafsi

01Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri azuia ‘malipo ya corona’ shule binafsi

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amepiga marufuku wamiliki wa shule binafsi kutaka kutoza malipo ya huduma ambazo hawakuzitoa kwa wanafunzi wakati wa mlipuko wa virusi vya corona.

Amesema kuwa serikali ndiyo iliyotangaza kuzifunga shule zote baada ya mlipuko wa virusi vya corona na yenyewe ndiyo imetangaza kuzifungua, hivyo wamiliki wa shule hizo wanapaswa kutii amri hiyo ya Rais John Magufuli.

Profesa Ndalichako alitoa angalizo jana alipohojiwa na Kituo cha Redio ya Clouds FM baada ya kuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya wazazi kuhusu kutopokewa shuleni kutokana na kutokamilisha malipo ya ada na michango mingine.

Waziri huyo pia alikemea kitendo cha baadhi ya wamiliki wa shule binafsi kuwataka wazazi walipie huduma ambazo hazikutolewa na shule zao kwa wanafunzi kipindi cha corona.

“Ni maagizo ya serikali wanafunzi wote warudi, Profesa Ndalichako alisema, "kwa hiyo wanafunzi waliondoka shuleni kwa amri ya serikali na wanatakiwa kurudi shuleni kwa amri ya serikali, tena iliyotangazwa na Rais.

"Tumeweka bayana kwamba ada kwa mwaka, kwa sababu masomo yatakamilika, itabaki palepale, lakini masuala ya usafiri kwa mfano wanafunzi 'wanachajiwa' hela ya usafiri siku ambazo hakuwapo shuleni wakati walikuwapo nyumbani, 'wanachajiwa' kwa misingi ipi?" Profesa Ndalichako alihoji.

"Ugonjwa kwa sasa hivi umepungua. Kwa hiyo, maelekezo ya Rais wanafunzi wote warudi shuleni na sisi tumesimamia wanafunzi wote warudi shuleni. Sasa watakapofika shuleni, kama mlikuwa mnadaiana na hamkufukuzana kabla ya corona, basi mtafukuzana watakapofika shuleni," alisema.

Katika hatua nyingine, Profesa Ndalichako amesema matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ulioanza juzi, yatatoka baada ya mwezi mmoja na wiki mbili tangu kukamilika kwake Julai 17 mwaka huu.

“Serikali imejipanga vizuri, wanafunzi watakaomaliza kulingana na ndoto zao, serikali iko tayari kutekeleza ndoto zao,” alisema, huku akiwataka wasimamizi kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuwa serikali haitamvumilia yeyote atakayekwenda kinyume cha taratibu.

Machi 17 mwaka huu, siku moja baada ya kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza wa corona nchini, serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ilitangaza kufunga shule na vyuo vyote, ikiwa ni mbinu ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Imeandikwa na Magdalena Haule na Mary Mshami

Habari Kubwa