Waziri Bashungwa aagiza uzalishaji zaidi vitakasa mikono

26Mar 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri Bashungwa aagiza uzalishaji zaidi vitakasa mikono

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, jana amekutana na wazalishaji wa vitakasa mikono (sanitizer) ili kuweka mikakati ya pamoja na kuongeza uzalishaji kutokana na tishio la ugonjwa wa corona.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, picha mtandao

Akifungua kikao hicho, Bashungwa alisema chimbuko la kikao hicho ni kutokana na ziara aliyoifanya kwenye maduka na viwanda vinavyotengeneza bidhaa hiyo na kubaini kuwapo uhaba wa vitakasa hivyo.

Alisema kikao hicho kitatoka na mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwa kuhakikisha vitakasa hivyo vinazalishwa kwa wingi na kukidhi mahitaji.

“Ili kupambana na ugonjwa wa corona ni kuzingatia kanuni za usafi, chimbuko la kikao ni ziara niliyoifanya Dar es Salaam kuangalia bei na upatikanaji wa vitakasa mkono lakini tulienda hadi viwandani, tuligundua kuna changamoto kwenye maduka na mikoa,” alisema.

Alisema pia katika ziara hiyo walibaini kuuzwa kwa bei kubwa na kulazimika kuitisha kikao hicho kujua kero wanazokabiliana nazo na uhitaji wa malighafi.

“Kupambana na corona kunahitaji ushirikiano wa pamoja na serikali, hivyo tuangalie serikali itimize majukumu yapi na wazalishaji mtimize wajibu gani,” alisema.

Alisema lengo ni kuhakikisha uzalishaji unaongezwa na kupatikana kwenye maeneo yote nchini na kwa wingi kutaondoa kero ya bei.

“Nilishaagiza Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Viwango nchini (TBS), kufanya msako nchi nzima ili kuwachukulia hatua wanaotaka kujitajirisha kwa mgongo wa Watanzania,” alisema.

Bashungwa alisema linatakiwa kuwapo soko huria la kuangalia utu na si kuwakomoa watu.

“Mwongeze uzalishaji wa vitakasa mikono na hata sabuni, upatikanaji wa ethanol, pale Tirdo wameanza tumewaambia wazalishe kwa wingi maana kuna kiwanda tulienda wakasema wanalazimika kuagiza ethanol nje ya nchi,” alisema.

Kadhalika alisema, kama wakizalisha kwa wingi wanaweza kuuza nje ya nchi.

Habari Kubwa