Waziri Hasunga awaalika wawekezaji kwenye kilimo

18Jun 2019
Nebart Msokwa
 MBEYA
Nipashe
Waziri Hasunga awaalika wawekezaji kwenye kilimo

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amewaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye kilimo cha mboga na matunda katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa kuwa mikoa hiyo ina fursa kubwa ya kuwekeza kwenye kilimo hicho ikiwamo ardhi yenye rutuba.

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Hasunga alitoa hamasa hiyo jana alipokuwa anafungua kongamano la kuhamasisha uwekezaji wa kilimo cha mboga na matunda lililoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (Sagcot) na Shirikisho la Wakulima wa Mboga na Matunda Tanzania (Taha).

Alisema katika mikoa hiyo kuna hali nzuri ya hewa na maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kwa sasa serikali imeweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji ikiwamo kuondoa baadhi ya kodi ambazo zilikuwa kero.

Alisema serikali inahimiza uwekezaji kwenye kilimo hicho baada ya kubaini kuwa kina manufaa makubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

"Taarifa zilizopo ni kwamba sekta hii ndogo ililiingizia taifa Dola za Kimarekani milioni 764 mwaka 2017, ikilinganishwa na Dola milioni 64 mwaka 2015, sasa tunawahimiza wawekezaji kuendelea kuja kuwekeza ili kuimarisha zaidi," alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji wa Uwekezaji kutoka katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mnali, alisema lengo la kuandaa kongamano hilo ni kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na serikali za mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wameandaa ardhi ya kutosha kwa ajili ya wawekezaji watakaoonyesha nia ya kuwekeza hasa kwenye kilimo cha mboga na matunda.

Alisema TIC pamoja na wadau wengine wanalenga kukuza kilimo cha mazao hayo ili kiwe na manufaa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alisema katika mkoa huo kuna fursa kubwa ya uwekezaji kwenye kilimo cha mazao hayo ikiwamo miundombinu ya barabara na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.

Kongamano hilo la kuhamasisha uwekezaji linafanyika kwa siku mbili katika Jiji la Mbeya likiwahusisha wakulima na wawekezaji kutoka zaidi ya mataifa saba duniani ambao wanataka kuwekeza.

Habari Kubwa