Waziri Jafo awatega Ma-DC Ma-DED ukusanyaji wa mapato

25Nov 2018
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe Jumapili
Waziri Jafo awatega Ma-DC Ma-DED ukusanyaji wa mapato

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, ametaja Mikao mitatu iliyofanya vibaya ukusanyaji wa mapato ya ndani huku akiwataka viongozi wake kujitathimini kuhusu utendaji wao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya RaisTawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, akitoa taarifa ya robo ya makusanyo kwa kila Halmashauri na Mikoa kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani), ofisini kwake Jijini Dodoma jana. PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Jafo aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jijini hapa kuhusu taarifa ya ukusanyaji mapato ya robo mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Jafo aliitaja mikoa hiyo mitatu iliyofanya vibaya kwenye ukusanyaji wake wa mapato ya ndani kuwa ni Mtwara, Kigoma na Ruvuma huku akiwataka viongozi wa mikoa hiyo kujitathimini kwa kushindwa kufikia malengo.

Alisema mkoa wa mwisho kabisa kwenye ukusanyaji wa wake wa mapato ni Mtwara uliokusanya asilimia sita ukifuatiwa na Ruvuma ambao ni wa pili kutoka mwisho uliokusanya asilimia 11 na Kigoma asilimia 13.

Hata hivyo, alisema mikoa 10 imefanya vizuri kwenye ukusanyaji huo wa mapato ya ndani kwa kukusanya juu ya asilimia 20 ikiongozwa na Simiyu kwa asilimia 29.

Aliitaja mikoa mingine iliyofanya vizuri na asilimia kwenye mabano kuwa ni Manyara (28), Lindi (28), Mara (24), Pwani (23), Arusha (23), Njombe (22), Dodoma (22), Mwanza (21) na Geita (21).

Alisema taarifa hiyo ya fedha ilianza Julai Mosi hadi Septemba 2018 kwa kuainisha makisio ya mwaka na mapato halisi ya halmashauri.

Alisema katika mwaka huo wa fedha halmashauri zilipangiwa kukusanya Sh. bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani na hadi Septemba 30, zimekusanya Sh. bilioni 143.6 sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka.

Katika uchambuzi wa mapato ya robo ya kwanza mwaka huo wa fedha unaonyesha kuwa, jumla ya halmashauri 76 zimefanya vizuri kwa kukusanya zaidi ya asilimi 20.

Alizitaja halmashauri zilizofanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato na asilimia kwenye mabano kuwa ni Jiji la Dodoma (21), Kinondoni (21) na Ilala asilimia 20.

Aidha, Jafo alisema halmashauri 23 mchini zimefanya vibaya kabisa kwenye ukusanyaji wake wa mapato kwa kukusanya chini ya asilimia 10 ya makisio yake ya ndani ya mwaka.

Alizitaja halmashauri tatu zilizofanya vibaya kabisa kwenye ukusanyaji wake wa mapato kuwa ni Masasi (asilimia mbili), Nanyamba na Nanyumbu zote za mtwara kwa asilimia tatu kila moja.

Waziri Jafo alisema Tamisemi imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kuunganisha halmashauri zote 185 mchini.

Aliowaonya baadhi ya wakuu wa wilaya na wenyeviti wa halmashauri kuwa wamekuwa kikwazo kwa kuzuia ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao.

Aliwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa wanasimamia ukusanyaji wa mapato na watakaoshindwa kufanya hivyo watapimwa utendaji wao.

Habari Kubwa