Waziri Lugola akipa neno kitengo cha malalamiko

19Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waziri Lugola akipa neno kitengo cha malalamiko

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, ametoa wito kwa watumishi wa Wizara hiyo kitengo cha kushughulikia malalamiko ya wananchi, kutekeleza wajibu wao wa kufuatilia na kuyapatia ufumbuzi wa haraka malalamiko wanayopokea.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Lugola aliyasema hayo jijini Dodoma juzi katika kikao kazi kilichoshirikisha watumishi wa kitengo hicho.

Aliwataka wafuatilie malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi ya taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

“Hakikisheni malalamiko mnayoletewa mnayapatia ufumbuzi wa haraka bila kufika ngazi ya juu, tekelezeni wajibu wenu kwa ufanisi ili kujenga imani kwa wananchi (walalamikaji).

“Kama wananchi watajiridhisha kuwa kitengo hiki ni msaada mkubwa kwao, mtakuwa mmejijengea uaminifu na kuifanya Wizara ijitegemee kushughulikia malalamiko,” alisema.

Lugola alisisitiza umuhimu wa viongozi wanaoshughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi kuchukuliwa hatua kama itabainika wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Alisisitiza umuhimu wa kubadili mfumo wa kushughulikia malalamiko akisema yanapofikishwa katika kitengo hicho yachunguzwe hapo hapo wizarani.

“Malalamiko yasirudishwe kwenye taasisi zinazolalamikiwa kama Polisi, Uhamiaji, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na NIDA…pia walalamikiwa waitwe na kuhojiwa.

Aliongeza kuwa, malalamiko mengine hayapaswi kuchukua muda mrefu ili kutatuliwa, akitolea mfano malalamiko ambayo aliyapokea kwa wananchi na kuyapatia ufumbuzi wa haraka kwenye ziara alizofanya katika mikoa mbalimbali.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, aliwapongeza watumishi wa kitengo hicho kwa kuyafuatilia malalamiko yanayotolewa na wananchi pamoja na kuyafanyia kazi kwa haraka.

Alisema kitendo cha kupokelewa, kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi ndani ya muda mchache, kitawezekana kama kila mtumishi anayeshughulikia malalamiko atawajibika ipasavyo ili kupunguza mrundikano wa malalamiko yanayotolewa.

Habari Kubwa