Waziri Lukuvi apokea msaada wa kompyuta

11Jul 2020
Munir Shemweta
Dodoma
Nipashe
Waziri Lukuvi apokea msaada wa kompyuta

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amepokea msaada wa kompyuta 10 zenye thamani ya milioni 12 kutoka Benki ya Azania.

Msaada huo ulipokewa jana katika Ofisi za Ardhi Mkoa wa Dodoma na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa wizara akiwamo Katibu Mkuu, Mary Makondo.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Waziri Lukuvi aliishukuru Benki ya Azania kwa msaada huo alioueleza kuwa utasaidia kwenye huduma za sekta ya ardhi, hasa katika ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni.

Alisema Benki ya Azania imekuwa ikiunga mkono jitihada za wizara kusaidia vifaa na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa benki hiyo kusaidia juhudi za serikali kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa wizara yake baada ya kuanzisha ofisi za ardhi katika mikoa, inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ofisi hizo zinakuwa na vifaa vya kutosha kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa ofisi hizo kufanya kazi kwa ufanisi.

Meneja wa Benki ya Azania Mkoa wa Dodoma, Makalla Mbura, alimweleza Waziri Lukuvi kuwa msaada uliotolewa, ni moja ya juhudi za benki hiyo kusaidia jitihada mbalimbali zinazofanywa na wizara kwenye sekta ya ardhi.

Makalla aliongeza kwa kusema kuwa, benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za wizara katika masuala mbalimbali ya huduma za sekta ya ardhi kwa kutoa msaada pale unapohitajika

Habari Kubwa