Waziri Lukuvi atumbua maofisa watatu ardhi

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe Jumapili
Waziri Lukuvi atumbua maofisa watatu ardhi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewasimamisha kazi watumishi watatu wa ardhi katika Jiji la Arusha kwa tuhuma za kushirikiana na matapeli wa viwanja.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, picha na mtandao

Aidha, Lukuvi ameagiza maofisa hao waliosimamishwa kazi kutokanyaga katika eneo la ofisi za jiji mpaka uchunguzi utakapofanyika na uamuzi dhidi ya tuhuma zao kutolewa.

Maofisa ardhi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.

Lukuvi alichukua uamuzi huo juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha kutokana na kuwapo tuhuma nyingi za matapeli ya viwanja kushirikiana na baadhi ya maofisa ardhi wasio waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali wa viwanja.

Mbali na kusimamishwa kazi kwa watumishi hao Waziri Lukuvi aliagiza maofisa ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao hawapatiwi huduma katika masuala yoyote ya ardhi.

Katika ziara yake hiyo ya kushtukiza pamoja na kuelezwa na Ofisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha, Dicley Nyato, uwepo wa watumishi wawili Lassen na Zawadi huku Elizabeth akiwa katika likizo ya uzazi, watumishi hao walipotea ghafla ofisini bila taarifa baada ya kuelezwa kuwa wanahitajika kwa waziri. Hata walipopigiwa simu za mkononi hawakupatikana.

Kwa mujibu wa Lukuvi, watumishi hao wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja katika jiji hilo, jambo linalotia mashaka utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa wamekuwa na tabia ya kufuatilia kesi zilizoko katika Mabaraza ya Ardhi kwa nia ya kuwasaidia matapeli.

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Lukuvi aliagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa mahakama zinazohusu masuala ya ardhi na nyumba, kutiwa saini na ama Ofisa Ardhi Mteule, Msajili wa Hati au Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda na kwamba Mwanasheria wa Wizara lazima afahamishwe uwapo wa kesi husika.

"Kuanzia sasa ‘summons’ hati za mahakama zote zipokewe na maafisa ardhi wateule, makamishna au wasajili wa hati wa kanda na watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha," alisema.

Lukuvi alisema matapeli wa viwanja wamekuwa wakifungua kesi katika mabaraza ya ardhi dhidi ya wamiliki halali na wakati mwingine matapeli hao hawawafahamu hata wamiliki lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda mrefu, ikizingatiwa baadhi ya wamiliki hawana uwezo wa kuweka mawakili, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.

Alisema tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa na kusisitiza kuwa, mtandao wote wa matapeli wa viwanja katika jiji la Arusha ataukomesha kama alivyofanya katika jiji la Dar es Salaam ambao awali ulishamiri.

Kwa upande wake, Nyato alimueleza waziri Lukuvi kuwa wamekuwa wakisumbuliwa sana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo na wakati mwingine matapeli hao huwashitaki lengo likiwa kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kuviuza.

Habari Kubwa