Waziri Mhagama awaomba wadau kuboresha taasisi za watu wenye walemavu

16May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waziri Mhagama awaomba wadau kuboresha taasisi za watu wenye walemavu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia kuboresha miundombinu katika vyuo vya ufundi vya watu wenye ulemavu ambavyo vipo katika kanda zote hapa nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akihutubia katika hafla ya kukabidhi mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation. Wengine ni Naibu Waziri wake (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof, Jamal Katundu (kushoto) na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa (wa kwanza kulia).

Ametoa wito huo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipokuwa akipokea mabweni mawili katika Chuo cha Ufundi Stadi kwa watu wenye ulemavu cha Yombo ambayo yamefanyiwa ukarabati na Shirika lisilo la kiserikali la Nyota Foundation kwa gharama ya Shilingi milioni 80.

“Sisi kama serikali tumejitahidi sana kuboresha vyuo hivi lakini niwaombe wadau wengine, makampuni, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa waviangalie sana vyuo vyetu. Vyuo hivi vinakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu mbalimbali pamoja na upungufu wa miundombinu muhimu vikiwemo vyoo, madarasa, mabweni na miundombinu nyinginezo,” amesema Mhagama.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akishiriki kukata utepe kama ishara ya kupokea mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation. Alioambatana nao ni Naibu wake, Ummy Nderiananga, Naibu Katibu Mkuu, Prof. Jamal Katundu, Wawakilishi kutoka Nyota Foundation pamoja Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, kwa takwimu za mwaka 2019/2020, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu milioni 55.9; Kati ya idadi hiyo, watu milioni 2.5 ni wenye ulemavu na hivyo kuongeza mahitaji ya huduma na miundombinu kwa ajili ya kundi hilo.

Awali, akimkaribisha Waziri Mhagama katika hafla hiyo, Naibu wake anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, alimpongeza kiongozi huyo wa Wizara kwa kujitoa kwake katika kuboresha mazingira na hali za watu wenye ulemavu kupitia kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa ameongozana na wawakilishi wa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo wakati wa hafla ya kupokea mabweni ya chuo hicho yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation.

Mwakilishi wa Shirika la Nyota Foundation, Zainab Mvungi, ameishukuru serikali kwa kuruhusu ukarabati huo kufanyika pamoja na kutoa ushirikiano wakati wote walipokuwa wakifanya kazi hiyo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, katika hafla ya kupokea mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo kinachomilikiwa na serikali kilianzishwa mwaka 1973. chuo hicho ambacho ni kwa ajili ya Kanda ya Mashariki ni miongoni mwa vyuo sita  ambavyo vipo katika kanda mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Vyuo vingine vipo Kanda ya Kusini (Mtwara), Magharibi (Tabora), Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Tanga) na Kati (Singida).

Habari Kubwa