Waziri Mhagama awasihi wanawake kushiriki Uchaguzi Mkuu

13Jul 2020
Dotto Lameck
Dodoma
Nipashe
Waziri Mhagama awasihi wanawake kushiriki Uchaguzi Mkuu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Jenista Mhagama, amewasihi wanawake kujitokeza kwa wingi katika kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini na kuepuka kusubiri nafasi maalumu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wanawake wa vyama vya siasa.

Mhagama amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na viongozi wanawake wa vyama vya siasa, huku akiwataka wanawake kusimama kidete katika kusimamia amani na kuwa chachu ya utulivu kwenye uchaguzi mkuu ujao na wasikubali kutumika na vyama vyao au wanasiasa kuvuruga amani.

Viongozi hao wanawake wamekutana na Waziri Mhagama kwa lengo la kumpogeza kwa kusimamia vema vyama vya siasa ambapo wizara yake ndio inayohusika na usimamizi wa vyama vya siasa kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Waziri Mhagama amesema wanawake wana nguvu kubwa na uwezo wa kuwa viongozi bora na ndio maana Rais Magufuli amewaamini na kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi na hata wakati alipoteuliwa tena na chama chake kuwa mgombea Urais wa CCM alimchagua tena Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake kwa mara nyingine.

" Nguvu yetu wanawake ni kubwa sana na kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi nitoe rai kwenu kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vyenu, chukueni fomu mkachuane kwenye majimbo na kata msiogope kwa sababu uwezo tunao”

 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akizungumza katika mkutano huo wa Waziri Mhagama na Viongozi Wanawake wa vyama vya Siasa nchini.

“Tusikubali kusubiri nafasi za upendeleo kama tuna lengo la kufikia 50/50 basi inatulazimu pia tuingie kwenye uwanja wa mapambano ili tupime nguvu zetu, na kwa sababu sisi tuna uwezo mkubwa basi naamini tutashinda," amesema Mhagama.

Nae Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi hao kutoruhusu kuwa sehemu ya machafuko yanayosababishwa na baadhi ya wanasiasa wasio na uzalendo wa nchi yao.

" Niwapongeze kwa Umoja wenu huu kama viongozi wanawake, mmekuja hapa pamoja mkiwa mmevaliwa sare moja ambayo siyo ya vyama vyenu, niwasihi Umoja huu huu ndio muende nao kwenye uchaguzi mkiweka mbele maslahi ya nchi yetu," amesema Jaji Mutungi.

 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akizungumza katika mkutano huo wa Waziri Mhagama na Viongozi Wanawake wa vyama vya Siasa nchini.

Habari Kubwa