Waziri Mkumbo asema  hakuna upungufu wa saruji

16Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waziri Mkumbo asema  hakuna upungufu wa saruji

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amewatoa hofu wananchi kwamba hali ya upatikanaji wa saruji nchini ni ya kuridhisha na viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa sasa vinatosheleza uhitaji wa nchi.

Prof. Mkumbo aliyasema hayo jana alipotembelea Kiwanda cha Saruji cha Twiga, Dar es Salaam ili kujiridhisha na uzalishajii na upatikanaji wa saruji.

Ziara hiyo inatokana na Tanzania kunufaika mkopo wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zitatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo kuboresha huduma za jamii katika sekta za afya, elimu, utalii na maji.

"Niwahakikishie Watanzania hali ya upatikanaji wa saruji nchini ni mzuri kulingana na uhitaji wa saruji na viwanda tulivyonavyo hakuna changamoto" alisema Prof. Mkumbo

Prof. Mkumbo alisema kuwa hali ya umeme katika viwanda inaendelea kuboreka lakini bado kuna changamoto kidogo.

Kutokana na hali hiyo, alisema atakutana wa Waziri wa Nishati, January Makamba ili kuhakikisha tatizo la umeme katika kiwanda cha Twiga na viwanda vingine nchini linakwisha kabisa.

Prof. Mkumbo pia alikutana na kufanya mazungumzo na mjumbe wa kampuni iliyowekeza katika kiwanda hicho kutoka Ujerumani ili kujadili maendeleo ya kiwanda na kumpa uhakika kuwa serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wao ambao wamefanya na wanaendelea kupanua.

Habari Kubwa