Waziri Mkuu aionya TCU kunyanyasa wanaosoma nje

18Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Mkuu aionya TCU kunyanyasa wanaosoma nje

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kukaa na taasisi zinazojishughulisha kupeleka Watanzania nje ya nchi kusoma masomo ya elimu ya juu na kufanyia kazi malalamiko yao.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mita ya maji ya malipo ya kabla, iliyobuniwa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph, Khadija Mustapha (kulia), kabla ya kufungua Maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: OWM

Amesema kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wanafunzi hao kuwa wanaporudi nchini, tume kutovitambua vyuo walivyosoma.

Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Maonyesho ya 14 ya Vyuo Vikuu yaliyoandaliwa na TCU na kuvishirikisha vyuo mbalimbali.

“Bado tuna tatizo, Mkurugenzi wa TCU, nilikudokeza kwamba wiki mbili zilizopita nilikuwa Misri nilipata fursa ya kuongea na Watanzania miongoni mwao ni wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma nchini humo,” alisema na kuongeza:

“Miongoni mwa malalamiko ni chuo kikuu (anakitaja) inaonekana Watanzania wanaosoma hapo wakimaliza na kupata vyeti vyao havitambuliki na TCU, kuna idadi kubwa ya Watanzania wanasoma hapo.

“Upo umuhimu wa kuona kwa nini cheti hicho hakitambuliki na kama havitambuliki kwa nini wanawapeleka Watanzania pale? Na cha ajabu zaidi ni kwamba miongoni mwao ni wale ambao serikali imewadhamini kwenda kusoma hapo,” alisema.

Majaliwa alisema ni muhimu TCU iangalie na kutatua changamoto hiyo ili serikali isije ikapoteza fedha hivyo wawaelekeze Watanzania waende kusoma vyuo ambavyo vinatambulika.

“Ninaielekeza TCU, tunatambua zipo taasisi binafsi zinazoshiriki katika kuwaelekeza na kuwatafutia nafasi Watanzania kwenda kusoma vyuo vya nje, ni muhimu mkazitambua taasisi hizi, tujue nani anafanya kazi kuwasaidia kupata vyuo nje, ni vyema na wao wapewe jukumu la kuanza kuhakiki ubora wa elimu waliyonayo kabla ya kuwaruhusu kuingia chuo kikuu, badala ya kuendelea kuorodhesha orodha na kuwapeleka nje kusoma shahada wakirudi hawatambuliwi kwa sababu hawana sifa,” alisema.

Majaliwa aliitaka TCU ikae na taasisi hizo, izisajili na kuzitambua kuwaambia mahitaji ya kwenda chuo kikuu ni yapi ili nao washiriki kuwashauri vijana sifa zinazotakiwa.

“Tume itafute mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili. Ni wakati mwafaka kwa tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hii,” alisema.

Pia Majaliwa aliitaka TCU itafute mbinu bora zaidi na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili kwa sababu lengo la serikali ni vishiriki katika maendeleo kwenye sekta ya elimu ya juu nchini.

“Tume itafute mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili. Ni wakati mwafaka kwa tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto zinazovikabili,” alisema.

Kuhusu idadi ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu alisema takwimu za kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonyesha kwamba kufikia mwaka 2017 ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania kwa kila Watanzania 100 wenye umri chini ya miaka 25 wanapata elimu ya Chuo Kikuu.

“Idadi hii ni ndogo zaidi ya majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne na Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na mikakati ya kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na majirani zetu,” alisema.

Alisema ili kuongeza idadi hiyo ni lazima wapange mikakati kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwa sababu kati ya wahitimu wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu binafsi.

Majaliwa amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu wabadilishe mtazamo wao kuhusu upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania badala ya kutumia machapisho ya kitaaluma.

Pia alisema utafiti unaofanywa vyuoni ulenge kutatua changamoto na kufanya mageuzi ya kiuchumi.

 

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema katika chapisho la mwaka 2016/17 la Benki ya Dunia (WB) kuhusu idadi ya maombi ya hati miliki zilizowasilishwa na nchi mbalimbali, Tanzania ilipeleka tatu tu wakati Kenya zilikuwa 135, Algeria 147, Misri 918, Ethiopia 12.

“Ninawaagiza wahadhiri na wakuu wa vyuo waangalie tatizo ni nini, je, ni elimu kuendelea kuwa na mwenendo duni,” alisema.

Mwenyekiti wa TCU, Prof. Jacob Mtabaji, aliwataka wahitimu wa kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu, wasome kwa umakini mwongozo uliowekwa kwenye tovuti na wasikubali kupitia mawakala wanaodai kuwa wanaweza kufanya usajili kwa niaba yao. Pia aliwataka wazingatie kalenda ya udahili.

Prof. Mtabaji alisema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa katika vyuo vikuu vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo wawasomeshe wahadhiri katika ngazi mbalimbali ili wakirudi wajiunge na vyuo husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, alisema taasisi 81 za elimu ya juu zimeshiriki maonyesho hayo na taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi 66 ni za hapa nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Watendaji Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki (CVCPT), Prof. Raphael Chibunda, aliishukuru serikali kwa uboreshaji uliofanywa kwenye upatikanaji na upelekaji kwa wakati wa fedha Bodi ya Mikopo kwa sababu awali lilikuwa  chanzo cha migomo mingi vyuoni.

Habari Kubwa