Waziri Mkuu awataka mabalozi kuhamasisha uwekezaji

17Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Waziri Mkuu awataka mabalozi kuhamasisha uwekezaji

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali watoe msukumo Katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi, kuimarisha biashara pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika maeneo yao ya uwakilishi.

Waziri Mkuu amekutana na mabalozi hao leo Januari 17, 2022 ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, ambapo pia amewasisitiza mabalozi hao kulinda taswira ya Tanzania katika nchi za uwakilishi.

Mabalozi aliokutana nao ni pamoja na Balozi Profesa Adelardus Kilangi (Brazil), Balozi Said Juma Mshana (DR-Congo), Balozi Alex Gabriel Kalua (Israel), Balozi Said Shaib Mussa (Kuwait) na Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta (Urusi).

Aidha, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakutane na Watanzania wanaishio nje ya nchi (Diaspora) na wawasaidie kuimarisha Jumuiya zao kwa kuwa na uongozi imara.

“Waunganisheni ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na kwenye shughuli za kijamii mnazozifanya huko.” Amesema Waziri Mkuu.

Habari Kubwa