Waziri Mkuu Salim avunja ukimya

07Feb 2016
Efracia Massawe
Nipashe Jumapili
Waziri Mkuu Salim avunja ukimya

WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye si mzungumzaji wa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari amewahamasisha Watanzania kuwekeza katika kilimo cha uyoga, ili kuinua uchumi wa familia zao na wa nchi kupitia zao hilo.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Utafiti cha Kilimo cha Uyoga kinachomilikiwa na taasisi ya Shirika la Afya na Elimu la Kairuki (KHEN). Dk. Salim alisema kama serikali itatoa hamasa kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika zao hilo, watu wengi watalima na linaweza kuleta manufaa makubwa ndani na nje ya nchi. Alisema zao hilo ni miongoni mwa mazao yasiyopewa kipaumbele na watu wengi nchini kutokana na wengi wao kutojua umuhimu wake mwilini, lakini wakipewa elimu kuhusu faida zake wanaweza kunufaika kupitia chakula na tiba pia. Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Profesa Keto Mshigeni, alisema katika kuenzi huduma za mwasisi wa taasisi hilo, Hubert Kairuki, kupitia maadhimisho ya 17 tangu mwasisi huyo alipofariki dunia, walibuni mradi wa kisasa wa kumnyanyua mwananchi wa kawaida kiuchumi. Alisema zao la uyoga likitumiwa vizuri mbali na kutumika kama chakula, ni miongoni mwa tiba nzuri kwa wagonjwa wanaotumia dawa za kuongeza kinga mwilini (ARV) pamoja na wale wa saratani. Alisema katika nchi zilizoendelea ikiwamo China, inayozalisha tani milioni 30 kila mwaka za Uyoga na kusambaza duniani, watu wengi huthamini kilimo hicho. “Wito wangu kwa watanzania ni kwamba tujenge desturi ya kulima kilimo cha uyonga kama mazao mengine makuu ya kunyanyua kipato cha taifa na mtu mmoja mmoja, nasema hivyo kwa sababu nina uhakika wanaweza kubadilisha maisha yao kupitia zao hilo,” alisema Profesa Mshigeni.

Habari Kubwa