Waziri Mkuu: Watanzania tununue bidhaa za ndani

04Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Mkuu: Watanzania tununue bidhaa za ndani

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa, amewataka Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, ili kukuza viwanda vya ndani na kuuinua zaidi uchumi wa nchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (wa pili kushoto), wakipata maelezo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia), kabla ya kufungua maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Meneja wa Benki hiyo, Kanda ya Mashariki, Badru Idd. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Majaliwa alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa anafungua Maonyesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara, maarufu Sabasaba, yakiwa na washiriki 2,880 wa ndani na nje ya nchi waliojitokeza kuonyesha bidhaa zao.

Alisema serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha bidhaa za ndani zinaboreshwa sambamba na kuboresha mazingira ya uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.

Alisema serikali itaendelea kuongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ili bidhaa za ndani zipate soko la uhakika.

“Muhimu kwetu ni kuhakikisha tunasimamia maendeleo yetu na kutatua matatizo yanayowakabili wafanyabiashara wa ndani na hivyo kuzalisha na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema.

Majaliwa alizitaka taasisi zinazojihusisha na utafiti, ziendelee kufanya kazi yake, ili kuwa na suluhisho la kudumu la matatizo yanayozikabili bidhaa za ndani.

Mtendaji mkuu huyo wa shughuli za serikali alipongeza jitihada zilizokuza sekta ya sanaa, burudani na michezo nchini, akibainisha kuwa sekta hiyo kwa sasa inatisha kwa kasi ya ukuaji nchini.

Katika hatua nyingine, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limepeleka huduma yake ya ‘T-Burudani’ katika maonyesho hayo.

Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Puyo Nzalayaimisi, alisema jana kuwa, Watanzania watakaotembelea maonyesho ya mwaka huu ndani ya banda lao, watajipatia huduma ya T-Burudani yenye ofa ambayo inatamwezesha mteja kupakua, kuhifadhi na kuangalia filamu aipendayo hata bila ya kuwa na mtandao wa intaneti.

Aliwaomba wananchi hasa wapenzi wa filamu nchini, kufurahia ofa hiyo ya Sh. 2,000 na kujipatia huduma ya T-Burudani toka TTCL itakayomwezesha mteja kuangalia filamu na tamthilia aipendayo bila ya kuwa na mtandao wa intaneti.

“Huduma ya T-Burudani ya TTCL ni rahisi, inamwezesha mteja kupakua filamu bila kutumia kifurushi cha intaneti, mteja ataweza kuangalia filamu zote za ndani ya nchi na kimataifa, mteja ataweza kupakua kupitia simu janja ya mkononi pamoja na kompyuta ya kiganjani,” alisema.

Nzalayaimisi alisema TTCL imeweka mfumo rahisi utakaomwezesha mteja kupakua filamu aitakayo kutokana na maudhui anuai duniani ikiwa ni pamoja na Hollywood, Nollywood, Bollywood, HBO, na Bongo Movies.

Aliongeza huduma nyingine ambazo TTCL inazitoa katika viwanja vya Sabasaba ni pamoja na huduma za usajili laini kwa wateja, kurudisha laini zilizopotea, vifaa vya internet kama modem na vinginevyo, huduma za T-PESA, huduma za mkongo wa taifa wa mawasiliano na huduma za Data Senta.

Habari Kubwa