Waziri Mpina adai kuhujumiwa

06Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Waziri Mpina adai kuhujumiwa

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amewashutumu baadhi ya viongozi wa serikali kwa kile alichodai kuhujumu opereshani ya kulinda rasilimali za serikali, huku baadhi yao wakidhani jukumu hilo ni la wizara pekee.

waziri wa mifugo na uvuvi luhaga mpina akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya tathmini ya matokeo ya operesheni nzagamba awamu ya pili jijini DODOMA, PICHA NA MTANDAO

Akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili iliyofanyika kwa siku 50 jijini Dodoma, Waziri Mpina alisema Katiba ya Tanzania, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na sheria za nchi vyote vimeelekeza cha kufanya kuhusu ulinzi wa rasilimali za taifa.

Kutokana na hali hiyo, alisema kiongozi yeyote anayekwamisha ulinzi wa rasilimali hizo, anavunja katiba na kudharau maagizo ya Ilani ya CCM pamoja na kupuuza maagizo ya Rais John Magufuli kuhusu msimamo aliouweka kwenye serikali kuhusu ulinzi wa rasilimali za taifa ikiwamo mifugo.

“Saa nyingine viongozi tuliopewa dhamana tunayabinafsisha mambo hii ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania. Kama Mpina unamwona ni mtu mdogo sana basi fuata Katiba inaelekeza nini ufanye kwenye ulinzi wa rasilimali za taifa. Ukimkingia kifua anayevunja sheria unakwenda kinyume cha Katiba, Ilani ya CCM, sheria na kuhujumu msimamo wa Rais Magufuli kuhusu jambo hili,” alisema.

Mpina alisema kama viongozi wote watakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya ulinzi wa rasilimali za taifa, ni dhahiri hakutajitokeza mtu au kiongozi yeyote tena wa ngazi yoyote, kupinga kusimamia mipango na shughuli zinazotekelezwa na serikali katika ulinzi wa rasilimali za taifa.

Kutokana na changamoto za usimamizi dhaifu wa biashara ya mifugo na mazao yake, Waziri Mpina ameanzisha kanda tano za ukaguzi wa rasilimali za mifugo ambazo ni Mashariki, Kati, Kaskazini, Ziwa na Kusini.

Pia aliagiza kuanzishwa vituo tisa vya ukaguzi wa mifugo, ili kusogeza usimamizi wa biashara ya mifugo katika maeneo ya Longido, Loliondo, Sirari, Babati, Mkwaja, Mikese, Nderema, Horohoro na Ochuna.

Katika hatua nyingine, Mpina alimwagiza Katibu Mkuu Mifugo kuondoa urasimu uliopo sasa wa  utoaji vibali wa kusafirisha mifugo kwenda nje ya nchi.

Pia alimtaka Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Wakala wa Usajili wa Majina ya Biashara (Brela) kusogeza karibu huduma ya utoaji leseni za biashara ya mifugo kuliko ilivyo sasa leseni zinapatikana Dar es Salaam yaliko makao makuu ya wakala huo.

Pia Waziri Mpina aliagiza watumishi wote wa Wizara ya Mifugo walioko kwenye kituo cha ukaguzi wa Kibaha waondolewe mara moja na kuteuliwa wengine kutokana na waliokuwapo kuonyesha udhaifu mkubwa katika usimamizi wa majukumu yao.

Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema operesheni hiyo imeendeshwa kwa mujibu wa sheria na kwamba inalenga kudhibiti utoroshaji wa mifugo na chakula cha mifugo kwenda nchi jirani.

Pia alisema operesheni hiyo inalenga kudhibiti uingizaji holela wa mifugo na mazao yake kutoka nje ya nchi, kulinda viwanda vya ndani, kulinda walaji na wazalishaji, kulinda ajira na kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.

Habari Kubwa