Waziri Ndaki awaondoa hofu wafugaji

09Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Waziri Ndaki awaondoa hofu wafugaji

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amesema serikali inawajali wafugaji ndiyo maana inaendelea  kuwawezesha wafanye shughuli zao kwa tija.

Ndaki aliyasema hayo juzi katika ziara yake Morogoro na Pwani ambayo lengo lilikuwa kutembelea maeneo yaliyokumbwa na ukame na kuathiri ustawi wa mifugo nchini.

"Rais wetu anawajali wafugaji ndiyo maana anafanya kila linalowezekana, ikiwamo kuipatia fedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwawezesha wafugaji kufanya shughuli zao kwa tija," alisema Ndaki.

Alisema katika kuhakikisha wafugaji wanaendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi, Rais Samia amezielekeza wizara nane chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuvibakisha katika maeneo vijiji 920 ambavyo vilikuwa na migogoro.

"Mheshimiwa Rais ameielekeza Wizara ya Ardhi kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kuwabakisha wale wanaoishi katika vijiji hivyo. Robo tatu ya maeneo yote ya vijiji hivyo wanakaa wafugaji," alisema.

Pia alisema Rais Samia ameridhia kwamba baadhi ya vijiji ambavyo maeneo yalichukuliwa na kufanywa eneo huru la uwindaji, yarudishwe kwa wanakijiji ili wayatumie kwa matumizi mengine.

"Nipende kuwahakikishia wafugaji kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza utaratibu wa kuyarasimisha kisheria kwa kuyatangaza kwenye  Gazeti la Serikali maeneo yote yaliyotengwa  kwa ajili ya wafugaji kwenye wilaya zenu," alibainisha.

Hata hivyo aliwatahadharisha wafugaji hao kutoingia katika vyanzo vya maeneo ya maji, maeneo tengefu kwa sababu yanalindwa kisheria, hivyo ni makosa kuingiza mifugo yao.

Awali, mmoja wa wafugaji kutoka Kijiji cha Kiwege, Kata ya Ngerengere mkoani Morogoro, Seif Lekake, alimweleza Waziri Ndaki kuwa ukosefu wa miundombinu na ufinyu wa maeneo kwa ajili ya kufugia, unachangia mifugo kuingia katika maeneo ambayo si ya ufugaji.

"Mheshimiwa Waziri tunahitaji msaada wako ili haya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya wafugaji yatafutiwe namna ya kupimwa ili yalindwe kisheria yasiendelee kumegwa kwa sababu baada ya muda yatapotea na wafugaji wataendelea kutangatanga," alisema Lekake.

Naye Kaimu Katibu wa Chama cha Wafugaji wilayani Kibaha, George Mfuko, alisema pamoja na ukame uliyoikumba nchi, matatizo makubwa wanayokumbana nayo ni maeneo ya kufugia na maji ya kunyweshea mifugo.

Kutokana na matatizo hayo, alimwomba waziri kuwawekea miundombinu ya maji ili mifugo iwe na uhakika wa maji.

Habari Kubwa