Waziri Ndalichako atimiza ahadi ya vyerehani 10

02Jul 2020
Dotto Lameck
Katavi
Nipashe
Waziri Ndalichako atimiza ahadi ya vyerehani 10

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ametimiza ahadi ya vyerehani 10 kwa wanafunzi waliohitimu mafunzo ya ushonaji kutoka Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Mpanda wanaotoka katika mazingira magumu.

Akizungumza katika halfa hiyo mkoani humo, Profesa Ndalichako amesema ahadi hiyo aliitoa mwaka 2018 baada ya kuwakuta vijana wadogo wamemaliza masomo ya darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari na kujiunga na mafunzo ya ushonaji katika chuo hicho kupitia msaada wa kanisa.

“Mwaka juzi nilifika katika chuo hiki na kuwakuta hawa vijana wawili wadogo wakiwa katika mafunzo ya ushonaji na nilipozungumza nao niligundua kuwa wametoka katika mazingira magumu, hivyo kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari, ndipo nilipowaahidi kuwapatia vyerehani watakapomaliza ili viwawezeshe kujiajiri. Hata hivyo, nimetoa vyerehani 10 ili na wengine wenye mazingira ya namna hiyo waweze kupata,” amesema Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri huyo amemuagiza Mkuu wa chuo hicho kuangalia namna ya kuwapatia nafasi ya kuendelea na ngazi nyingine ya mafunzo watoto hao ili kuwawezesha kuwa mahiri katika ushonaji na kuhakikisha anawasimamia na kuwashauri popote watakapokuwa wanafanya shughuli zao.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Elisha amemshukuru Waziri kwa kutimiza ahadi aliyoitoa mwaka 2018 kwani inakwenda kuinua watoto wanaotoka katika familia masikini, na kuahidi kuendelea kuwasimamia ili cherehani hizo ziwe na manufaa kwa watoto wenyewe na familia zao.

Habari Kubwa