Waziri Ummy aagiza masoko yote yawe na visima vya maji

11Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waziri Ummy aagiza masoko yote yawe na visima vya maji

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, ameagiza kuwa masoko yote yanayomilikiwa na Halmashauri hususani masoko makubwa pamoja na stendi zote ziwe na visima vya maji vitakavyowezesha kukabiliana na majanga ya moto yanayotokea mara kwa mara.

Ummy Mwalimu.

Ummy amesema hayo baada ya kukatisha ziara yake ya Kigoma na kuja mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia ajali ya moto ambayo imetokea katika soko kuu la Kariakoo jana.

Amesema kuungua kwa soko hilo kumetoa msukumo mkubwa wa kujenga soko lingine kubwa mkoani humo ambalo litakuwa ni zaidi ya soko la kariakoo.

“Soko hili limejengwa mwaka 1971 na likafunguliwa mwaka 1975, ukiangalia idadi ya watu wa Dar es Salaam kipindi hiko na idadi ya watu sasahivi, kwetu sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia halmashauri zetu kuungua pia kwa soko hili imetupa msukumo wa kujenga soko kubwa Dar es Salaam ambalo litakuwa ni zaidi ya soko la kariakoo” amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa pole kwa wafanyabiashara zaidi ya 224  ambao wameathirika na janga hilo kubwa la moto

Habari Kubwa