Waziri Ummy aijia juu NHIF kulipa malipo huduma kwenye hospitali

22Mar 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Ummy aijia juu NHIF kulipa malipo huduma kwenye hospitali

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameutaka mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) walipe ndani ya mwezi mmoja malipo ya huduma zinazotolewa kwenye hospitali nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Ameyasema hayo leo Machi 22, 2019 jijini Dar es salaam wakati akizindua jengo la huduma binafsi katika hospitali ya CCBRT ambalo litasaidia kutoa huduma za kibingwa na kuendesha huduma nyingine zinazotolewa hospitali hapo.

" NHIF najua mnajificha kwenye kivuli cha kudai mnahakiki, haya ni maelekezo hakikisheni hili linafanyiwa kazi na nilishamwambia Mkurugenzi. Hospitali mkimaliza huduma za mwezi mpeleke kwa wakati NHIF na nyie NHIF msiwe kikwazo cha huduma bora,  hospitali wanategemea fedha hizi kulipa mishahara, kuendesha huduma, kununua dawa na vitu vingine, sitaki kusikia watu wanalalamika kuwa hawataki kupokea kadi kwa sababu ya malipo mnayachelewesha,"

Ummy amesema hayo baada ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, kueleza kuwa hiyo ndiyo changamoto wanayokutana nayo katika utoaji wa huduma kwenye jengo la huduma binafsi lililozinduliwa leo CCBRT, Dar es Salaam.

Pia Waziri Ummy, amesema wagonjwa wa festula wamepungua kwa sababu vituo 350 vimeboreshwa nchini kutoa huduma bora za uzazi.

Amesema wamepunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 40 kuanzia mwaka 2012 hadi 2018.

Waziri Ummy amesema ndani ya wiki tatu serikali itatangaza vifurushi vya bima ya afya kwa mtu mmoja mmoja lengo kuhakikisha watanzania wawe na bima ya afya kwa sababu ndio njia rahisi itakayowawezesha watanzania kupata huduma kwa urahisi.

Habari Kubwa