Waziri Ummy amsimamisha kazi msimamizi stendi ya mabasi mwenge

20Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waziri Ummy amsimamisha kazi msimamizi stendi ya mabasi mwenge

​​​​​​​WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amemsimamisha kazi Mhandisi Isack Mpaki, aliyekuwa anasimamia miradi mitatu ya Manispaa ya Kinondoni ikiwemo ujenzi wa stendi ya mabasi mwenge, ujenzi wa uwanja wa mpira Mwenge na ujenzi-

-wa jengo la utawala la Manispaa ya Kinondoni baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Waziri Ummy amechukua uamuzi huo leo Juni 20, 2021 mara baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa Stendi ya Mabasi Mwenge Jijini Dar es Salaam ambapo ujenzi huo unajengwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa mfumo wa Local Fund ( Force Account) ambao ulianza Aprili 2020.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo Waziri Ummy amesema kuwa ili aweze kujiridhisha ni lazima iundwe timu ambayo itaweza kuchungunza ujenzi wa mradi huo ili aweze kutoa tamko rasmi na ujenzi ukaendelea.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema amepata malalamiko na jumbe nyingi kutoka kwa wakazi wa Manispaa ya Kinondoni hususani Wananchi ambao walikuwa wanatumia eneo hilo wakilalamika kusuasua kwa ujenzi wa stendi hiyo ambayo ilitakiwa imalizike Mei 2, mwaka huu.

“Kuna figisufigisu kwenye huu mradi haiwezekani tukawa tunatupiana mipira kwahiyo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi Prof.Shemdoe nataka Jumanne aniletee timu huru ya kuja kuchunguza mikataba yote” amesema Waziri Ummy.

Habari Kubwa