Waziri Ummy awaibukia ‘wazungusha raundi’ baa 

06Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Waziri Ummy awaibukia ‘wazungusha raundi’ baa 

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewaasa wanywaji  pombe kuacha kuzungusha raundi baa badala yake wawekeze kwa watoto kwa kuwawekea akiba benki kwa maisha yao ya baadaye.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Ummy alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa elimu ya fedha kwa ajili ya watoto na vijana iliyoandaliwa na Benki ya NMB.

NMB kupitia kampeni yake ya Wajibu inamaanisha ‘Wajibika’ ni mpango wa elimu kwa wanafunzi na wazazi unaojumisha akaunti tatu za akiba ikiwamo NMB Mtoto, NMB Chipukizi na NMB Mwanachuo.

 Ummy alisema kabla baba hajaenda baa kuzungusha raundi 10 za bia, anapaswa kujiuliza kama mtoto wake ana akaunti.

“Pia kwa mwanamke badala ya kumtunza shoga yako beseni lililosheheni vitu vya Sh. 200,000, hakikisha kwenye fedha hiyo unatoa ya kumwekea akiba mtoto wako.

“Watanzania tujifunze kuweka akiba za watoto wetu. Fedha unazotumia kwa mambo yasiyo na mpango  kwa ajili ya mtoto wako, njoo NMB fungua akaunti ya mtoto akaunti, Chipukizi au Mwanachuo Akaunti,” alisema.

“Hakuna mtoto wa taifa la kesho, kesho inaanza leo. Kwa hiyo kama inaanza leo, anza kuweka akiba kwa ajili ya kesho,” alisema Ummy.

Waziri huyo alisema takwimu zinaonyesha Tanzania ina watoto milioni 25 na  kama kila mzazi ataamua kumfungulia akaunti mtoto wake na kumwekea Sh. 50,000 ina maana watapata jumla ya Sh. bilioni 500.

Kadhalika aliipongeza benki hiyo kuhusiana na kampeni yao ya Jifunze, Jipange na Wajibika na kueleza kuwa ni ya umuhimu kwa sababu inawakumbusha wazazi namna ya kuweka akiba za watoto.

Alisema pamoja na kwamba serikali imeweka elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne haimaanishi kuwa mzazi hachangii chochote.

“Yapo baadhi ya mambo ambayo mzazi anaingia gharama kuchangia kwa hiyo kama mtoto akiwekewa akiba hakutakuwa na changamoto,” alisema.

Alisema amekubali kuwa balozi wa kampeni hiyo ya elimu ya fedha na kueleza kuwa katika kuhamasisha umma kuwafungulia watoto wao akaunti, ataanza na familia yake.

“Nitakuja kabla ya mwisho wa mwaka huu kufungua akaunti za watoto wangu wawili, mmoja nitamfungulia mtoto akaunti na mwingine chipukizi akaunti,” alisema.

Alisema takwimu za Benki Kuu Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa idadi ya wanaotumia huduma za kibenki zimeongezeka ambapo mwaka jana walikuwa asilimia 9.1 na mwaka huu wamefikia asilimia 16.7.

Katika hatua nyingine, Ummy ameiomba benki hiyo iweke utaratibu wa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili wakati wakihamasisha watu kufungua akaunti za watoto, wawe na utaratibu wa kuwawezesha kupata kadi za bima ya afya za ‘Toto Afya Card’.

“Ombi langu kwenu tukae pamoja na mfuko wa taifa wa bima ya afya ili tuhamasishe watu wakifungua akaunti za watoto, kuwe na utaratibu wakifikisha kiasi cha kufungulia bima ya afya, utaratibu ufanyike wapewe kadi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema akaunti hizo za aina tatu ni mahususi kwa vijana ambao wengi wao ni wale walioko mashuleni kwa ajili ya kuwasaidia wajiwekea akiba na kupanga matumizi yao.

Pia alisema benki hiyo inatambua kupanua elimu ya fedha ni muhimu ili kuweza kutumika kikamilifu kunufaisha uchumi jumuishi.

Kadhalika, alisema benki hiyo imeongeza uelewa kuhusu akaunti ya Chipukizi ili kuongeza kupatikanaji fedha kwa vijana ili kusaidia kutimiza malengo yao na kujijengea tabia ya kujiwekea akiba.