Waziri Ummy awasimamisha kazi Wakurugenzi wawili

25Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Waziri Ummy awasimamisha kazi Wakurugenzi wawili

​​​​​​​WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu, amewasimamisha kazi wakurugenzi wawili wa Halmashauri kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo tuhuma za ubadhirifu na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo.

Ummy Mwalimu.

Kutokana na taarifa iliyotolewan leo April 25, 2021na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (Tamisemi), Nteghenjwa Hosseah, amesema Waziri Ummy amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) kupeleka timu ya uchunguzi mara moja katika Halmashauri hizo.

Waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli.

Waziri Ummy amemsimamisha Mwakabibi baada ya kupokea malalamiko na tuhuma kutoka kwa wananchi na viongozi juu ya mwenendo wake usiofaa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na usimamizi usiofaa wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Temeke.

Mwakibibi amekuwa na mgogoro pia na waandishi wa habari kwa muda sasa kwa sababu ya kukataa kutoa taarifa mbalimbali anazoulizwa na siku chache zilizopita, aliamuru kukamatwa kwa waandishi wawili kwa madai waliingia kwenye mkutano wake na wafanyabiashara bila idhini yake.

Pia, Waziri Ummy amemsimamisha Msemakweli ni kutokana na tuhuma za ubadhirifu, usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo na uhusiano usioridhisha kati yake na madiwani, mkuu wa wilaya na viongozi wengine wa wilaya na wa Mkoa wa Rukwa.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wakurugenzi na watendaji wote wa halmashauri kuheshimu mipaka yao ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na amewaasa kuwa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kufanya ubadhirifu na kukiuka sheria.

Habari Kubwa