WCF yatwaa tuzo Sabasaba

15Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
WCF yatwaa tuzo Sabasaba

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), umetwaa tuzo ya mshindi wa kwanza ya Mwonyeshaji Bora Kundi la Taasisi za Bima na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam, maarufu Sabasaba.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Masha Mshomba, alipokea tuzo hiyo kutoka kwa Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, wakati wa kilele cha maonyesho hayo kwenye Viwanja vya Julius Nyerere jana.

“Kusema kweli siku ya leo (jana) tunayo furaha sana. Mimi mwenyewe na wafanyakazi wenzangu wote kwa mara ya kwanza tumeshika nafasi ya kwanza katika sekta ya bima na mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Hii inadhihirisha kwamba penye nia pana njia. Mwaka jana, tulikuwa washindi wa pili, tukaweka azma kwamba walau siku moja tuwe washindi wa kwanza na leo imefika, tunashukuru sana.

"Ushindi huu unaendana na dira yetu ya mfuko, tumejiwekea malengo ya kuwa taasisi ya kuigwa siyo tu hapa Tanzania, bali Afrika hususan katika taasisi za hifadhi ya jamii na haswa katika mifuko ya fidia na tunapokuwa wa kwanza katika maonyesho haya makubwa nchini, hiyo inaonyesha kwamba tuko katika njia sahihi na lengo letu ni kuendelea kushika nafasi kama hizi katika maonyesho na shughuli mbalimbali tunazoshiriki.

“Huduma zetu ni bora, tumeboresha sana huduma zetu na kwa sasa zinapatikana kupitia mtandao na waliofika katika banda hili wameelezea jinsi walivyovutiwa na huduma zetu zote zinazopatikana kupitia mtandao na ule usumbufu kwa wateja haupo kabisa kwa sababu mafao yanalipwa kupitia mtandao."

Mkurugenzi huyo alisema taarifa za kutokea ajali au kuumia kazini pia zinawasilishwa kupitia mtandao sambamba na usajili wa waajiri na wanachama wenyewe.

"Kila kitu kwa sasa tunafanya kupitia mtandao. Usajili wa waajiri ni kupitia mtandao, ukusanyaji wa michango ni kupitia mtandaoni. Kwa hiyo, kila kitu tunafanya kwa kutumia mtandao na hilo kwa kweli limewezesha kuboreshwa kwa shughuli zetu na nia yetu ya kuwa kileleni," alitamba.

Habari Kubwa