Wema aachiwa huru, kisha akamatwa tena

05Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wema aachiwa huru, kisha akamatwa tena

SAKATA la kesi ya kuchapisha picha za ngono iliyokuwa inamkabili  msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu (30), limechukua sura mpya  baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumwachia huru kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuita mashahidi.

Mahakama hiyo ilimwachia Wema jana chini ya Kifungu cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) 225 kifungu kidogo cha (5) sura ya 20,  lakini alikamatwa tena.

Uamuzi huo ulitolewa jana saa 4:40 asubuhi katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde.

Kabla ya uamuzi huo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Glory Mwenda, ulidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba shahidi waliyemtegemea, mpelelezi Koplo Safi ni mgonjwa.

Alidai kuwa wanawategemea mashahidi wawili na kwamba  mbali ya Koplo Safi, shahidi mwingine yuko jijini Arusha, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Mawakili Albart Msando na Rubern Semwanza, ulipinga ombi la Jamhuri.

Msando alidai kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya mahakama hiyo, ilipotoa uamuzi wake mwezi uliopita, ilisema kwamba katika kutenda haki inazingatia hoja za pande zote mbili yaani Jamhuri na utetezi.

Alidai kuwa upande wa Jamhuri ulipaswa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha kwamba shahidi ni mgonjwa na lini atahudhuria kesi hiyo.

Pia alidai kuwa mpaka sasa hakuna hati ya kiapo cha Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) cha kuomba kuongezewa siku 60.

"Mahakama hii haiwezi kumnyima haki mshtakiwa chini ya kifungu cha 225 kidogo (5) cha CPA na uamuzi huo hauwezi kuunyima haki upande wa Jamhuri kumfungulia upya mashtaka pale watakapokuwa tayari kuendesha kesi hii," alidai Msando wakati akiwasilisha hoja za kuomba mteja wake kuondolewa mashtaka.

Akijibu hoja za utetezi, Wakili Mwenda alidai kuwa suala la ugonjwa ni la kibinadamu, shahidi alipokea hati ya wito wa mahakama lakini ameshindwa kwenda mahakamani kwa sababu ya ugonjwa.

Kuhusu kiapo cha RCO cha kuongeza muda, alidai kuwa kinatumika pale upelelezi unapokuwa haujakamilika lakini kesi hiyo inasikilizwa.

Akisoma uamuzi wake, Hakimu Kasonde alisema amesikia hoja za pande zote mbili, kifungu kinachomtaka RCO kuongeza siku 60 kinatumika kabla ya upelelezi na wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Alisema Machi 19, mwaka huu, kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa lakini ilipigwa danadana mpaka Aprili 18, mwaka huu na mahakama yake ilitoa ahirisho la mwisho.

"Tangu mahakama yangu itoe ahirisho la mwisho mpaka leo (jana) ni miezi miwili. Maofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walibaini tukio la mshtakiwa kupitia mtandao wa Instagram wakalijulisha Jeshi la Polisi lakini mpaka leo (jana) hawajafika kutoa ushahidi," alisema na kuongeza:

"Mahakama ina muda wake wa kusikiliza kesi kuendelea kumshikilia mshtakiwa wakati ana majukumu mengine kama kilimo, biashara na mambo mengine yanayoongeza uchumi na ujenzi wa taifa si sahihi. Nakubaliana na ombi la utetezi, namwachia chini ya kifungu cha 225 kidogo cha (5) cha CPA," alisema Hakimu Kasonde Msando.

Hata hivyo, saa 4:43 baada ya kuachiwa, alikamatwa na askari polisi kisha alipandishwa kwenye gari lenye namba za usajili SKA 535 M aina ya Toyota Landcruser na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (ZCO) Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Saa 6:15 mchana  akizungumza na Nipashe, Wakili Msando alisema polisi wamemwachia huru na kwamba watakapomhitaji watamjulisha.

Akiwa nje ya viunga vya Mahakama ya Kisutu, baada ya kuachiwa, Wema alisema anamshukuru Mungu amefurahi ameachiwa dhidi ya kesi hiyo.

Wema aliyekuwa ametinga suti ya suruali ya rangi ya kaki na shati jeupe lenye vidoti vya rangi ya zambarau na viatu vya mchuchumio vyeusi, alifurahia kuwa huru dhidi ya tuhuma hizo.

Katika kesi ya msingi, alikuwa anatuhumiwa  kuwa Oktoba 15, mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Habari Kubwa