Wema aswekwa mahabusu siku 7

18Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wema aswekwa mahabusu siku 7

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeamuru  msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu (30), kupelekwa mahabusu mpaka Juni 24, mwaka huu, itakapotoa uamuzi ama afutiwe au aachiwe kwa dhamana baada ya kushindwa kufika kusikiliza kesi yake.

Mahakama hiyo imeamuru Wema kupelekwa mahabusu jana baada ya mshtakiwa huyo kwenda kujisalimisha na kujieleza kwamba alishindwa kufika mahakamani Juni 11, mwaka huu, kutokana na maradhi ya tumbo.

Wema anayekabiliwa na mashtaka ya kuchapisha video ya ngono katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, aliamriwa kwenda mahabusu na Hakimu Mkazi Maira Kasonde, anayesikiliza kesi hiyo.

Kabla ya amri hiyo, Wema aliieleza mahakama  kwamba Juni 11, ilikuwa siku ya kusikiliza kesi yake, lakini alipofika viunga vya mahakama hiyo alipata maradhi ya tumbo ghafla, hivyo  akalazimika kwenda hospitalini.

"Mheshimiwa naomba mahakama yako inisamehe kwa sababu nilikuwa naumwa tumbo na Juni 14, mwaka huu nilishindwa kuja nilikwenda Morogoro kikazi, nilimpa taarifa wakili wangu," alidai Wema.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Glory Mwenda, alidai kumbukumbu za mshtakiwa huyo katika kuhudhuria mahakamani ni nzuri, lakini alitakiwa  kuwaagiza wadhamini wake ili kuiepushia mahakama usumbufu.

"Nimesikia hoja za pande zote mbili. Mahakama  yangu itatoa uamuzi Juni 24, mwaka huu, na kwa sababu suala hili linahusu dhamana, mshtakiwa atakwenda rumande mpaka siku ya uamuzi wa mahakama hii," alisema Hakimu Kasonde.

Juni 11, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa Wema baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Silvia Mintanto, kuomba hati ya kukamatwa msanii huyo.

Wakili wa utetezi, Reuben Semwanza, alidai kuwa mshtakiwa alifika mahakamani kusikiliza kesi yake lakini alipatwa na ugonjwa wa ghafla.

Habari Kubwa