Wengi watinga kwa mkemia kujua uhalali baba wa mtoto

12Dec 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wengi watinga kwa mkemia kujua uhalali baba wa mtoto

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Kati, imesema asilimia 90 ya sampuli za kupima vinasaba (DNA) ilizozipokea, zililenga kuangalia uhalali wa baba wa mtoto.

Meneja wa kanda hiyo, Musa Kuzumila, aliyasema hayo jana alipozungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka miwili na nusu tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo katika ziara ya timu ya maofisa habari wa wizara na taasisi zake mkoani Dodoma.

Alisema kati ya sampuli mbalimbali 5,106 zilizokusanywa kwa kipindi hicho, 36 zililenga kuangalia uhalali huo, akieleza kuwa majibu ya sampuli hizo husaidia kumaliza kesi au migogoro kwa wakati.

“Hapa sina takwimu sahihi za kina baba wangapi wamesingiziwa watoto ambao si wao, tumekusanya sampuli 36 za DNA, asilimia 90 kati ya hizo ni za kusaka uhalali wa baba wa mtoto.

“Huwa tunapeleka kuchunguza kwenye maabara zetu zilizopo Dar es Salaam na Mwanza, tumekusanya na kufanya uchunguzi sampuli 5,106 hadi Desemba hii.

"Tunapofanya uchunguzi wa namna hii, DNA inahusika moja kwa moja na kutoa ushahidi mahakamani na kusaidia kesi kutatuliwa kwa wakati,” alisema.

Alibainisha kuwa asilimia kubwa ya sampuli zilizokusanywa, zilikuwa za dawa ya kulevya hususan bangi. Alisema sampuli za dawa hizo wamekuwa wakizipokea kwa kiasi kikubwa.

Habari Kubwa