Wengine 1,800 mikopo HESLB

13Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wengine 1,800 mikopo HESLB

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupata mikopo, ikiwa ni awamu ya nne.

Kutolewa kwa orodha hiyo mpya kunafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa kufikia 31,353.

Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, na kufuatiwa na 11,481 na kisha 7,901 katika awamu ya tatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).

Aidha, taarifa ya HESLB ilisema orodha kamili pia ilitumwa kwa vyuo husika jana ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.

“Tumekua tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa," ilisema taarifa ya HESLB ikimkariri Badru. "Leo (jana) tumetoa hao 1,775.”

Taarifa ya HESLB kwa vyombo vya habari pia ilikumbusha kuwa kiasi cha Sh. bilioni 427.54 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa Sh. bilioni 147.06 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/2018.

"Fedha hizo, Shilingi 427.54, ni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo."

Wakati huohuo, taarifa ya HESLB ilisema bodi hiyo imetangaza kufungua dirisha la rufani kuanzia leo hadi Jumapili ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufani kupitia vyuo walivyopata udahili.

Kwa mujibu wa taarifa ya HESLB, lengo la bodi hiyo ni kuhakikisha inatangaza majina yote ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufani zao ifikapo au kabla ya mwisho wa mwezi.

“Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufani za wanafuzi na kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kabla ya Novemba 22, 2017 ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufani zao ifikapo Novemba 30, 2017,” taarifa ilimkariri Badru akisema.

Habari Kubwa