Wenye kadi ya NHIF kuanza kutibiwa hospital za Aga Khan

05Mar 2019
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wenye kadi ya NHIF kuanza kutibiwa hospital za Aga Khan

MTANDAO wa Mashirika ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) umesema upo katika mazungumza na bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuwawezesha wenye bima hiyo kupata huduma katika hospitali zote walizonazo.

Mkurugenzi wa Tiba na Afya wa Taasisi ya utoaji huduma za afya Aga Khan Tanzania, Dk. Ahmed Jusabani, akizungumza na waandishi wa habari.

Hayo yamesemwa leo Machi 5, 2019 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tiba na Afya wa Taasisi ya utoaji huduma za afya Aga Khan Tanzania, Dk. Ahmed Jusabani, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa jengo jipya lilogharimu Sh bilioni 192 lililopo katika hospitali ya Aga Khan.

Amesema hospitali ya Aga Khan ilikuwa inapokea wagonjwa wa bima ya NHIF hadi mwaka 2012 ilipotokea tatizo wakasita kuendelea kutoa huduma kwa watu wenye bima hiyo.

“Baada ya hapo tulianza tena kuwapatia huduma, mwaka jana wagonjwa 300,000 walipatiwa huduma ya bima ya NHIF katika vituo vyetu zaidi ya 20 vilivyopo Dar es Salaam na mikoa mingine na kwa Dar es Salaam tunaendelea kuwapokea wagonjwa ambao ni wabunge. Sio kwamba tumekataa kupokea bima hiyo tupo kwenye majadiliano na bodi ya NHIF ,” amesema

Ameongezea kuwa:” Katika hospitali ya Aga Khani ya Dar es Salaam tunawapokea wabunge mazungungo ya bodi yanayoendelea yataelenza ni jinsi gani tuweze kuwapokea na wagonjwa wa kawaida na sio wabunge pekee,”

Amesema fikra iliyopo kwa sasa ni kila mmoja aweze kupata huduma katika hospitali ya Aga Khan wanachokiangalia ni  kuwepo na mfumo wa rufaa ili wale wanaostahili kufika hospitali hapo waweze kupatiwa huduma.

Aidha, amesema huduma wanaendelea kutoa kwa wenye bima ya NHIF na kwa mwaka huu wanategemea idadi ya wagonjwa kuongezeka huku wakiendelea na mazungumzo na bodi.

Aidha, amesema hospitali hiyo haina gharama kubwa ikilinganishwa na zile zinazotolewa nje ya nchi na mkakati wao ni kuhakikisha huduma zao zinawafikia wananchi wote.

“Huduma zetu ni za kawaida kuna vitu vya kuangalia tunaudhibitisho wa kimataifa wa kutoa huduma bora na salama, tumewekeza katika teknolojia ya hali ya juu tuna teknolojia ambazo hazipo katika hospitali nyingi za Tanzania, fani ambazo hazina madaktar bingwa hapa Tanzania imetubidi tuwachukue madaktari kutoka nje ya nchi,” amesema

Dk. Jusabani amesema kuna progaramu ambazo wameziweka katika hospitali hiyo ili wananchi wasiende nje ya nchi kutokana na gharama za nje ya nchi kuwa ni kubwa.

Aidha, amesema jengo hilo jipya litazinduliwa Marchi 9 mwaka huu na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, uzinduzi wa jengo hilo nisehemu ya kuongeza huduma za afya nchini.

 

Habari Kubwa