Wenye ualbino washauriwa kuepuka utegemezi

20Apr 2019
Peter Mkwavila
DODOMA
Nipashe
Wenye ualbino washauriwa kuepuka utegemezi

CHAMA cha watu wenye ualbino (TAS) kimeshauriwa kuibua miradi ili kuondokana na utegemezi unaowafanya kuwa maskini ikiwa ni pamoja na kuungana ili kuunda vikundi vitakayowawezesha kupata mikopo toka taasisi za kifedha.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Grace Products LTD Dk. Elizabeth Kilili, alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama cha walemavu wa ngozi Mkoa wa Dodoma, wakati wa ugawaji wa mafuta na sabuni kwa ajili ya kulainisha na kuondoa madoa kwenye ngozi jijini Dodoma.

Aidha, chama hicho kimetakiwa kufanya kazi kwa bidii na malengo ili waweze kujiinua kiuchumi.

Alisema ili waweze kufikia malengo hayo yote wao wenyewe wanatakiwa kutojikataa kutokana na maumbile kwa kujiona kama hawafai mbele ya watu wengine wasiokuwa na ulemavu huo.

"Ninawaomba mfanyekazi kwa ubunifu na msifanye kwa mazoea, kwa maana mkifanya kazi kama kawaida mtaendelea kuwa maskini na siku zote mtakuwa watu wa kuinyoshea serikali kuwa haiwatendei haki zenu za kimsingi wakati siyo kweli," alisema.

Awali Katibu wa TAS, Hudson Seme, alisema watu wenye ualbino wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikisababisha kuwapo kwa umaskini miongoni mwao.

Alisema hali hiyo imechangia wengi kushindwa kutunza ngozi zao hali inayowafanya kuwa na saratani ya ngozi.

"Moja ya changamoto tunayokabiliana nayo ni hili tatizo la kuwapo kwa umaskini kwenye familia tunazoishi nazo ukizingatia zilizo nyingi zina tatizo la kiuchumi na ndiyo maana tunashambuliwa na magonjwa hayo," alisema.

Katibu huyo pia aliwataka Watanzania kuwajali watu wenye ulemavu kuwasaidia mahitaji muhimu kama vitendea kazi ili waweze kujisimamia wenyewe.

Habari Kubwa