Wenye ulemavu wapewa mikopo ya bilioni 3

09Aug 2020
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Wenye ulemavu wapewa mikopo ya bilioni 3

Serikali imetoa mikopo isiyokuwa na riba yenye thamani ya shilingi bil 3.8 hadi kufikia Julai mwaka huu kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwainua kiuchumi ili kuwaondoa kwenye adha ya kuombaomba na kuwawezesha kuwa na shughuli za kufanya zinazowaingizia kipato.

Baadhi ya wahudumu Wa Afya ngazi ya jamii wakionesha namna vitimwendo vitakavyotumika kwa wenye ulemavu baada ya mafunzo ya mradi Wa Ulaya yanayofadhiliwa na World Vision.

Pesa hizo zimetokana na mikopo ya asilimia 2 iliyokuwa ikitolewa na kila Halmashauri nchini ambapo vikundi 370 vya watu wenye ulemavu tayari vimekopeshwa.

Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu, Philbert Kawemama, alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya wawezeshaji wa huduma za afya ngazi ya jamii chini ya mradi wa Ulaya unaofadhiliwa na World Vision Tanzania.

Kawemama alisema Serikali imedhamiria kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia Halmashauri zao kwa mikopo ya asilimia 2 ambayo haina riba.

Alisema ni jukumu la maofisa ustawi wa jamii kwa sasa kuhakikisha wenye ulemavu wanapata mikopo hiyo isiyokuwa na riba yoyote inayotolewa kila mwaka.

“Maofisa ustawi ni jukumu lenu muwaambie wenye ulemavu mikopo ipo, waitumie, wakope na kufanya biashara, waache kukaa na kuombaomba”  

Aidha alisema Serikali imeguswa zaidi na suala la kusaidia wenye ulemavu Vitimwendo (Baiskeli za wenye ulemavu) ambapo itahakikisha mradi huo unakuwa endelevu hata ufadhili utakapokwisha.

Naye Mratibu wa Mradi wa Ulaya, Chilala Elisei alisema, tayari vijana 32 wameshapewa mafunzo ya kuwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaoshirikiana na watendaji wa kata, mitaa na vijiji katika kuwapata wahitaji na kuwagawia vitimwendo 40 vyenye thamani ya shilingi mil 26 vilivyotolewa kwenye kata za Magole na Ulaya wilayani Kilosa mkoani hapa.  

Alisema viti hivyo vitagawiwa kwa walemavu maalum watakaothibitika kuwa na ulemavu wa kutumia viti hivyo ili kutimiza lengo maalum lililokusudiwa.

Aidha Elisei aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutambua kuwa wamebeba jukumu kubwa la jamii ambapo inawapasa kutunza siri za wateja wao kama wanavyofanya madaktari.

Alisema kufuatia mafunzo kwa wahudumu kugawanywa katika makundi matatu ya utambuzi, ufuatiliaji na tathmini wahudumu hao wanapaswa kuhakikisha wanayazingatia mafunzo hayo hasa kwenye utambuzi na kuweza kugawa viti hivyo bila kuwa na shida yoyote ikiwemo malalamiko ya upendeleo ili kusiwepo na dosari watakapopita kwenye ufuatiliaji na tahmini.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Sharifa Mjewa mkazi wa Magole aliishukuru World Vision Kwa mafunzo waliyowapa sambamba na vifaa vya wenye ulemavu ambapo ameahidi kwenda kutekeleza aliyofundishwa bila upendeleo.

Habari Kubwa