Wenye vyeti feki hawalipwi ng’o

24May 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Wenye vyeti feki hawalipwi ng’o

 SERIKALI haiwezi kuwalipa wale waliokumbwa kwenye sakata la vyeti feki ambao walikuwa wamekaribia kustaafu kwa kuwa walifanya kosa la jinai, Bunge lilielezwa jana mjini hapa. 

Aidha, imesema watumishi 1,907 waliokuwa wamekata rufani kutokana na kuondolewa kazini kwa vyeti feki wamerudishwa kazini. Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, alisema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya wabunge waliohoji kuhusu hatima ya watumishi waliokumbwa na kadhia ya vyeti feki kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Miongoni mwa wabunge hao ni Halima Mdee (Kawe- Chadema) ambaye alihoji ni kwa nini serikali haijawalipa watu walioondolewa kazini. “Hivi ni kweli serikali ya CCM inadhani ni sahihi kwa watu ambao wametumikia taifa kwa miaka 20 hadi 40 waondoke hivi hivi bila kupata kifuta jasho?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Kairuki alisema waliokata rufani na kurudishwa kazini ni 1,907 na suala hilo la kuwalipa kifuta jasho ni jinai na hawawezi kunufaika hata kama walipenya kwenye mfumo. “Suala hili halijazaliwa na serikali ya CCM bali ni kesi ya jinai na ilikuwa  lazima kufanya hivyo,”alisema Kairuki. Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Wingwi (CUF), Juma Hamad Kombo, alitaka kujua serikali kama ilipoteza watumishi 3,655 kwa mwaka 2017/18, imeajiri hadi sasa walimu wangapi. Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda, alisema baada ya uhakiki kukamilika kwa mwaka 2016/17 na 2017/18, imeajiri walimu 6,495.  “Kati yao walimu wa shule za sekondari wa masomo ya sayansi na hisabati ni 3,728 na walimu wa shule za msingi 2,767 na idadi hiyo ni zaidi ya walioachishwa kazi kwa ajili ya vyeti feki,”alisema. Katika swali la msingi, Mbunge wa Ziwani (CUF), Nassor Suleiman Omar, alitaka kujua wafanyakazi wangapi wamepoteza ajira katika sekta ya elimu kutokana na vyeti feki. Akijibu swali hilo, Kakunda alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18 serikali ilifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma ili kubaini waliokuwa na vyeti halali na waliokuwa na vyeti vya kughushi. “Katika uhakiki huo, jumla ya walimu 3,655 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi hivyo walipoteza sifa za kuendelea kuwa watumishi wa umma,”alisema. 

Habari Kubwa