Wenyeviti kamati nyeti Bunge wapinga serikali

17Apr 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Wenyeviti kamati nyeti Bunge wapinga serikali

WENYEVITI wa Kamati za Kudumu za Bunge za Serikali za Mitaa (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wamekosoa utaratibu unaotumiwa na serikali kujibu hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge akiwa na Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale Mwiru.

Tangu Alhamisi, mawaziri wamekuwa wakikutana na waandishi wa habari na kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na CAG katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni mjini hapa Jumatano, lakini kamati hizo zimedai utaratibu huo unakiuka taratibu.

Utaratibu huo mpya awali ulipingwa vikali na CAG mstaafu, Ludovick Utouh ambaye aliukosoa mwishoni mwa wiki iliyopita, na sasa wenyeviti wa PAC na LAAC ambao kwa taratibu za Bunge ndiyo kamati zinazoshughulikia ripoti za CAG wamekuja juu pia.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge mjini hapa, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alikosoa utaratibu mpya unaotumiwa na serikali kujibu hoja za CAG.

Kaboyoka aliyekuwa amefuatana na Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale Mwiru, alisema kinachofanywa na mawaziri kwa sasa ni sawa na kutoa maoni kwa kuwa sheria inawataka maofisa masuhuli wa wizara (makatibu wakuu) ndiyo waandae majibu ya hoja za CAG na kuyawasilisha bungeni ili yashughulikiwe na PAC na LAAC.

Kaboyoka alisema kitendo cha mawaziri kumjibu CAG kwa kuzungumza na vyombo vya habari ni kinyume cha taratibu za Bunge ambazo zinaelekeza kuwa PAC na LAAC ndiyo wanapaswa kuita taasisi zilizoguswa na kuzihoji kisha kutoa taarifa bungeni.

“Bunge linawajibika kusimamia matumizi ya fedha za umma na CAG ni jicho la Bunge, anaangalia kama hizi fedha zimetumika kama Bunge lilivyopitisha," Kaboyoka alisema na kufafanua zaidi:

“Bunge tusingeweza kukaa wote, CAG anavyopitia taarifa anarudisha kwa muhusika anawapa siku 21 kujibu, akimaliza akifunga mjadala analeta bungeni na yaliyo kwenye ripoti, ina maana ni hoja zilizoshindwa kujibiwa na wahusika, wakija hapa sisi tunawahoji."

Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), aliitolea mfano kauli ya Waziri wa Fedha  na Mipango, Dk. Philip Mpango ya ufafanuzi wa hoja ya CAG juu ya mafuta, iliyoelekezwa kwenye wizara yake.

Dk. Mpango aliwaambia waandishi wa habari kuwa mafuta hayo ambayo CAG alisema yalitakiwa yaende migodini lakini yakatumiwa na watu wengine, fedha zake zimeanza kurudishwa.

Lakini Mwenyekiti wa PAC huyo akahoji nani aliyethibitisha hilo. “Nani ahatakikisha hilo kwa sababu huku ni kumdhalilisha CAG, aonekane taarifa zake zimepitwa na wakati," alisema Kaboyoka.

"Kwenye kamati tungehoji zaidi hizi fedha zimerudishwa vipi.

“Kama tunataka hadhi ya Bunge ibaki ilivyo, taratibu zilizopo zifuatwe, kama tunataka kulidhalilisha, basi tuvunje taratibu.”

Kwa upande wake, Ngombale Mwiru alisema hoja yao kubwa ni kuona taratibu za kibunge zinafuatwa akieleza kuwa si utaratibu wala utamaduni mawaziri kufanya kinachoendelea sasa dhidi ya hoja za CAG.

Alisema taratibu za Bunge zinalekeza ripoti ya CAG ikishatolewa ipelekwe kwa maofisa masuhuli, na wakimaliza wairudishe kisha kamati ziwaite, kuwahoji na CAG akiridhika ndiyo afute hoja husika.”

WASIWE WEPESI

Awali Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, akitoa mwongozo kuhusu hoja ilitolewa juu ya jambo hilo, alisema kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo, wabunge wasiwe wepesi kuzungumza mambo ambayo hawajayapitia kisheria.

"Sisi tukizungumza tunaonekana tumetoa msimamo fulani kwa sababu ndivyo wananchi wanavyotuona maana sisi ndiyo wawakilishi wao," alisema.

"Kama ambavyo sheria haimkatazi CAG kuzungumza na vyombo vya habari, kwa namna hiyo hiyo haimkatazi yeyote kuizungumzia taarifa ya CAG."

Dk. Tulia alisema sheria haijasema CAG azungumze na vyombo vya habari na haijamkataza yeyote ikiwa ni pamoja waziri au naibu waziri kuzungumzia taarifa hiyo.

"Na ndiyo maana baadhi ya vyama vya kisiasa vimeshaielezea ripoti hiyo kwa vile inavyofaa. Sheria hizi mkizipitia, majibu huwa hayatolewi kwa mdomo.

Ukisema waziri anajibu hoja za CAG hayo ni mawazo yake lakini humu ndani (bungeni) anayeleta taarifa ya CAG ni waziri, ndivyo sheria inavyosema." 

Kiongozi wa Bunge huyo alieleza CAG hana mahali anapopeleka taarifa yake bungeni isipokuwa kupitia kwa waziri, hivyo mawaziri wanavyotoa maelezo si kwamba wanajibu hoja za CAG kwa kuwa hoja hizo zinajibiwa kwenye kamati kwa mujibu wa sheria.

"Anayejibu kwenye kamati ni ofisa masuhuli husika. Tusitake kuliweka hili jambo kuonyesha hakuna utawala wa sheria nchini. Sheria zipo tuzipitie kabla hatujatoa maelezo," alisema Dk. Tulia na kufafanua:

"Sheria iko wazi ikishaletwa hapa bungeni kila mtu yupo huru kuizungumzia kwa sababu ipo wazi kwa umma. Yanayojibiwa ni kwenye kamati na mengine ni maoni kama yanayotolewa na vyama ambavyo vimeshaisoma na kuitolea maoni yake."

UNGA MKONO

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe, aliunga mkono kauli iliyotolewa na Naibu

Spika, akisisitiza kuwa baada ya CAG kuzungumza na waandishi wa habari, wananchi wana haki ya kufahamu utekelezaji wa hoja hizo kutoka upande wa serikali.

"Kuhusu madai yaliyoibuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa tunachokifanya tunakiuka sheria, nimekuwa nikijiuliza sheria ipi? Na uzoefu wangu miaka mingi ya kubobea sheria, sijaiona hiyo sheria mpaka sasa," Dk. Mwakyembe alisema.

"Kwa kifupi, niseme madai hayo naomba muelewe yanapwaya na hayana mashiko kabisa kwa sababu ukiisoma kwa macho ya kisheria, Sheria ya Ukaguzi, Sura ya 418 kama ilivyorekebishwa na Bunge mwaka 2012, sheria hii inawataka maofisa masuhuli waandae taarifa ya kuelezea madhaifu yote aliyoelezea CAG katika maeneo yao."

Dk, Mwakyembe ambaye ndiye mwenyekiti wa mikutano ya mawaziri na waandishi wa habari kuzungumzia hoja za CAG, alisema taarifa hupelekwa kwa Katibu Mkuu wa Hazina na kila katibu mkuu ambaye kuna jambo lake limeguswa, anapaswa kutoa maelezo na mpango kazi wa namna ya kuyatatua kisha kumpelekea Katibu Mkuu wa Hazina.

"Sheria inamtaka Katibu Mkuu Hazina ajumuishe taarifa na mpango kazi kwa Waziri wa Fedha ambaye mpango kazi na majibu ya serikali atawasilisha bungeni," alisema Dk. Mwakyembe.

"Nikiwakumbusha kwamba kifungu cha 30(3) cha sheria hiyo kinasema bayana kuwa taarifa ya Waziri wa Fedha itawekwa mezani sambamba na taarifa ya ukaguzi ya CAG." 

Dk. Mwakyembe aliendelea kueleza kuwa kwenye taarifa ya shughuli za Bunge Aprili 11, mwaka huu (siku ambayo ripoti za CAG ziliwasilishwa), kulikuwa na taarifa sita za ukaguzi alizotoa Waziri wa Fedha kisha mwishoni aliwasilisha majibu ya serikali na mpango kazi wa utekelezaji wa mambo  yaliyoanishwa na CAG.

"Tulichofanya ni kueleza tunafanya hivi wala hatubishani na CAG, yeye ni msaidizi mkuu wa kazi tunazofanya kwa sababu ndiye anaainisha mapungufu yapo wapi na kazi yetu ni kufanyia kazi hayo mapungufu," alisema.

Alisema baada ya CAG kuweka taarifa yake mezani, aliongea na waandishi wa habari na waandishi wakapata picha ya sehemu moja tu ya kilichowekwa mezani bungeni.

"Sasa jamani kuna dhambi gani kuyafanyia kazi hayo masuala wakati hiyo ripoti ilikuwa mwisho ni Juni 30, mwaka jana. Hivi kweli serikali gani miezi 10 hakuna kilichofanyika? Yaani hiyo ndiyo wangefurahia kina Zitto (Kabwe).

Habari Kubwa