Wenyeviti mikoa Chadema wamtembelea Mbowe gerezani

18Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wenyeviti mikoa Chadema wamtembelea Mbowe gerezani

WENYEVITI wa mikoa mbalimbali wa Chama cha Deokrasia na Maendeleo (Chadema), wamemtembelea Mwenyekiti wa chama hicho taifa Freeman Mbowe, katika gereza la Ukonga ili kumjulia hali na kumtia moyo katika kesi inayomkabili.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa William Mungai.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Oktoba 18, mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa msafara huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoani Iringa William Mungai, amesema wamekuta Mbowe ana afya njema na yuko imara katika mapambano.

"Tumemuona Mwenyekiti yuko imara na ametuhakikishia kwamba afya yake ni njema katika mazingira aliyopo, yupo anajisomea vitabu, tunaamini akitoka atakuwa bora zaidi" amesema Mungai.

Aidha, Mungai amewataka wananchi waendelee kufuatilia kesi ya kiongozi huyo ambayo itaendelea Oktoba 2021 huku akisisitiza kwamba chama kitaendelea kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kwa sababu ndiyo mahitaji ya sasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Njombe Rose Mayemba, amesema licha ya Mbowe kushikiliwa mahabusu, bado chama hicho kiko imara kwa sababu alitengeneza viongozi wengine wenye uwezo wa kupambana kwa niaba ya wananchi.

"Mbowe kuwa gerezani, haijarudisha nyuma harakati za chama, tuko imara, tutaendelea kuwa imara na hii inatukumbusha Watanzania kwamba kama Mbowe, Mwenyekiti wa chama taifa anatiwa gerezani, wewe je? Uko katika hali gani?" alizungumza na anahoji mwenyekiti huyo.

Ifahamike kuwa Mwenyekiti huyo wa Chadema Taifa anakabiliwa na kesi ya ugaidi na leo ametimiza siku 90, tangu alipokamatwa akiwa mkoani Mwanza alipokuwa akiongoza kikao cha kuhamasisha kupatikana kwa katiba mpya.

Habari Kubwa