Wiki ya Maji, DAWASA yafungua dawati maalum kuhudumia wananchi

16Mar 2019
Frank Monyo
Dar es salaam
Nipashe
Wiki ya Maji, DAWASA yafungua dawati maalum kuhudumia wananchi

Katika maadhimisho ya wiki ya maji Duniani, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) imefungua dawati maalum kwa ajili ya kuhudumia wateja katika viwanja vya mnazi mmoja.

Afisa wa DAWASA Jamil Bakari akimpa maelekezo mteja aliyefika katika Banda la huduma kwa wateja katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika viwanja hivyo, leo Machi 16,2019 Mkuu wa Kitengo Cha Habari wa DAWASA, Neli Msuya, amesema katika maadhimisho ya mwaka huu DAWASA imejipanga kila idara kwa ajili ya kusikikiza na kero na changamoto za wateja na kuzitatua kwa wakati.

“Katika maadhimisho haya DAWASA imefungua dawati maalum kwa wateja ambalo ni dawati la Tehema, Miradi ya maji na dawati la Manispaa zote za jiji la Dar es salaam pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hivyo tunawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili tuwahudumie ,” amesema Msuya

Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yatahitimishwa Machi 22,2019 mkoani Dodoma ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni “Hakuna atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wore katika dunia inayobadilika kitabia nchi”

Ameongeza kuwa kesho Machi 17,2019 DAWASA itazindua mradi wa majitaka Temeke Wailes.

Amesema kuwa wananchi watakao fika katika katika viwanja vya Mnazi Mmoja watapata fursa ya kupata maelezo ya mipango inayoendelea kutekelezwa ili kuboresha sekta ya Maji Jiji la Dar es salaam na katika miji ya Mkoa wa Pwani.