Wizara ya Kilimo yaeleza mkakati kumaliza changamoto sekta ya mbolea

02Jul 2020
Mary Geofrey
DAR ES SAALAM
Nipashe
Wizara ya Kilimo yaeleza mkakati kumaliza changamoto sekta ya mbolea

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, amesema changamoto zinazowakabidili wawekezaji wa sekta ya mbolea nchini, zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuimarisha Sheria ya Mbolea namba 9 ya mwaka 2009 inayohusu uwekezaji na usimamizi wa mbolea nchini.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya.

Amesema sheria hiyo itaboreshwa kwa kuundwa jopo la wizara ili kuimarisha uhusiano na Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kusaya ameyaeleza hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao cha wadau wa chai kwa ajili ya kujadili mbolea ya Minjingu Chai zinazozalishwa nchini.

Amesema mpango huo utasaidia kutatua changamoto kubwa zinazowatesa wawekezaji wa mbolea ambazo ni gharama za uwekezaji zinazofanya mbolea zinazozalishwa nchini kuwa na bei kubwa kuliko zinazoingia nchini.Kusaya amesema pia kuwapo na mifumo ya kisheria yenye utata ambayo inamlazimisha mwekezaji kushughulikia masuala mengine yanayoweza kufanywa na taasisi nyingine.

Kadhalika amesema changamoto nyingine ni kukosekana kwa ushirikiano wa watengenezaji wa bidhaa saidizi kama watengeneza vifungashio na waweka maandishi kwenye vifungashio.

Kusaya amesema kwa sasa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini(TFRA), ina jukumu la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika viwanda na kuboresha sheria ya mbolea na miongozo inayohamasisha wawekezaji waliopo kuzalisha kulingana na uwezo wa kiwanda.

Ameeleza kuwa, TFRA inaendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba viwanda vyote vya mbolea na visaidizi vyake vinasajiliwa na kuwa na leseni hai muda wote.

Amesema TFRA inaendelea kufuatilia na kutoa ushauri kwa wawekezaji wa viwanda vya mbolea na kukamilisha nyaraka zote muhimu zinazotakiwa ili kukidhi vigezo vya kuanzisha viwanda vya mbolea.

Katibu Mkuu huyo amesema pia TFRA inashirikiana na Taasisi za utafiti na wadau wengine wa maendeleo katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea.

“TFRA inaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali wa kilimo kupitia vyombo vya habari na maonyesho ya kilimo ili waweze kuwekeza katika tasnia ya mbolea,” amesema Kusaya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk. Stephen Ngailo, amesema jumla ya upatikanaji wa mbolea nchini ni tani 544,162 sawa na asilimia 93 kwa mwaka 2019/20 wakati mahitaji ya nchi yalikuwa ni tani 586,604.

Amesema wanaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wanakidhi mahitaji yote nchini lakini pia kumaliza changamito zinazowakabili, wakulima, wazasindikaji wa kahawa na mbolea.

Habari Kubwa