Wizara ya mifugo yaanzisha kambi ya uhamilishaji

04Aug 2020
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
Wizara ya mifugo yaanzisha kambi ya uhamilishaji

Katika kuhakikisha teknologia mpya ya upandikizaji mbegu Ngo’mbe kwa njia ya mpira inawafikia wafugaji wengi zaidi nchini Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha kambi za uhamilishaji nchi nzima.

Mfugaji Nashoni Kilabu kutoka Wilaya ya Butiama Mkoani Mara akionesha ng' ombe ambao walipandikizwa mbegu kwa mpira.

Kambi hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani, kituo cha taifa cha uhamilishaji cha taifa, ambao wamekuwa wakitoa mafunzo ya teknologia hiyo kwa watalaamu wa mikoa na Halmashuari.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji Vina saba vya Mifugo na Uzalishaji, Abdallah Temba, wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima kitaifa (Nanenane) katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Temba amesema  kambi hizo zimeazishwa kwenye Mikoa ya Simiyu, Mara, Tabora, Katavi, Dodoma, Lindi, Kagera, Geita pamoja na Pwani ambapo zaidi ya Ngo’mbe 7000 wamepandikizwa kupitia kambi hizo.

Ameongeza  kuwa kupitia kambi hizo serikali ina uhakika kuwa migogoro ya wafugaji na wakulima itapungua nchini, kwani kwa kutumia teknologia hiyo wafugaji wataweza kufuga kisasa zaidi.

Mbali na kuanzishwa kwa kambi hizo, Temba amesema kuwa Wizara imeendelea kuboresha kituo cha uhamilishaji cha taifa kilichopo mkoani Pwani, ambapo kituo hicho kina madume 40 wenye uwezo wa kuzalisha mbegu za wafugaji wote nchi nzima.

Habari Kubwa