Wizara yatoa tahadhari kwa mvua zinazoendelea

16Oct 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wizara yatoa tahadhari kwa mvua zinazoendelea

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewatahadharisha wananchi kuzingatia kanuni za afya kutokana na mvua zinazonyesha baadhi ya maeneo ikiwamo Mkoa wa Dar es Salaam.

Kutokana na mvua hizo, wizara imesema kuna uwezekano wa kuibua magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, kuhara damu na yale yanayoenezwa na mbu kama vile malaria na dengue, iwapo tahadhari hazitachukuliwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, alisema uharibifu wa miundombinu umeanza kujitokeza ikiwamo ya kusafirishia na kuhifadhi majisafi na taka jambo, ambalo linahatarisha afya ya jamii.

“Kuna uwezekano mkubwa wa kusababisha kuenea kwa urahisi magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko. Kutokana na hali hiyo, wizara inatoa tahadhari kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa haya,” alisema.

Aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kushirikiana na viongozi wengine wa serikali za mitaa, wananchi na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kila eneo  haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko.

Prof. Makubi alizitaja kanuni wanazotakiwa kufuata wananchi ni pamoja na  kuchemsha maji ya kunywa, kuepuka kula chakula kilichopoa, au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.

Zingine ni kutumia ipasavyo, vyoo na kunawa mikono kwa maji safi na tiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutoka chooni, baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.

“Hatua zingine ni kuosha matunda na majisafi kabla ya kula, kuongeza usimamizi wa usafi wa jumla na mikono katika maeneo ya mikusanyiko kama shuleni, vyuoni na sokoni,” alisema.

Sambamba na hilo, aliwataka kutotapisha vyoo, kujikinga kuumwa na mbu pamoja na kutumia vyandarua, kusimamia usafi  katika mifumo ya majisafi, majitaka na mitaro.

 “Nawaomba sana waganga wetu wa wilaya wachukue ‘leadership’ (uongozi)  katika hili na kushirikiana na mamlaka ndani ya eneo lao. Wizara inaendelea kuwakumbusha tiba ni bora kuliko kinga,” alisema.
 

Habari Kubwa