Wizi vyuma chakavu wapatiwa ufumbuzi

12Apr 2017
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wizi vyuma chakavu wapatiwa ufumbuzi

SERIKALI inaandaa rasimu ya muswada wa sheria itakayoweka taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa biashara ya chuma chakavu, vikiwamo vya madaraja vinavyoibwa na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage.

Aidha, serikali imekiri kushamiri kwa biashara ya vyuma chakavu nchini hali inayosababisha kuwapo na uharibifu wa miundombinu inayojengwa kwa vyuma.

Hayo yalibainishwa jana bungeni na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum(CCM), Fakharia Shomar Khamis.

Mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipangaje kupambana na wizi na uharibifu wa mali za serikali zilizojengwa kwa vyuma.

“Biashara ya vyuma chakavu imeshamiri nchini na imesababisha madhara ya kuharibiwa na kuibiwa kwa miundombinu ikiwamo mifuniko ya chemba za majitaka, je, serikali haioni kwamba hata usalama wa raia na mali zao uko mashakani?” Alihoji Khamis.

Akijibu swali hilo, Mwijage alisema kutokana na mahitaji ya vyuma chakavu kuwa makubwa, wahalifu wanaharibu miundombinu kwa nia ya kupata chuma ili wauze kama chakavu.

Alisema miundombinu iliyoathirika ni mifumo ya kusafirisha umeme, reli, barabara na usambazaji maji.

Alisema ili kukabiliana na hujuma hizo, mamlaka husika za Tanesco, Tanroads na Rahaco wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi, ikiwamo kutumia walinzi kulinda rasilimali hizo.

“Ili kupata suluhu ya kudumu, wizara imekwishaandaa rasimu ya muswada huo ambao unadhibiti kuanzia uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya taifa,”alisema.

Aidha, alisema muswada huo utaweka bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu.

Aliwataka wenye viwanda na wafanyabiashara hiyo kujiepusha na ununuzi wa vyuma ambavyo asili yake ina mashaka.

Habari Kubwa