Wizi wa mafuta wamshtua Waziri

01Nov 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Wizi wa mafuta wamshtua Waziri

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, amevitaka vyombo vya ulinzi mkoani Kigoma kufuatilia wizi wa mafuta aina ya dizeli lita 23,000 yaliyoibwa kwenye ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu.

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa.

Kwandikwa aliyasema hayo jana wilayani Kasulu, Kigoma, alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu (km 63) inayojengwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation na kuelezwa kuwa kuna wizi wa mafuta uliofanyika hivi karibuni.

Aliwataka makandarasi na wasimamizi wa miradi kutoa elimu kwa waajiriwa kila siku kabla ya kuanza kazi na kukemea wizi na ubadhilifu wowote utakaotokea.

Aidha, aliwataka wananchi wanaopata nafasi za kazi katika miradi ya ujenzi wa barabara kuwa wazalendo katika kulinda vifaa na kuepuka vitendo vya hujuma.

"Wizi wa namna hii haukubaliki na mtandao ni mkubwa, hivyo naagiza vyombo vya usalama vichukue hatua kali mapema ili kuondoa madhara makubwa zaidi," alisema.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu inayojengwa kwa kiwango cha lami, Kwandikwa alielezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi ya mkandarasi huyo kwa kuwa mpaka sasa umefikia asilimia 52.

Kwandikwa alimtaka mkandarasi aendelee kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo kwa kuwatengenezea barabara nzuri ya mbadala hasa kipindi hiki cha mvua ili iweze kutumika kwa urahisi na kufanya wananchi kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.

Kwandikwa alisema nia ya serikali ni kufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami kwa kuwa ni kiungo kikuu kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi na Rwanda na mikoa yenye  uzalishaji mkubwa katika uvuvi, kilimo, madini na utalii.

Aidha, Kwandikwa alitoa wito kwa madereva nchini kuzingatia upakiaji wa mizigo kulingana na sheria na utaratibu waliopewa ili kuweza kuzilinda barabara zetu nchini zinazojenga kwa fedha nyingi.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, alisema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh. bilioni 60 ambazo zote ni fedha za ndani na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani.

Alisema barabara hiyo pindi itakapokamilika itafungua fursa za ajira na uchumi na kuunganisha mkoa wa kigoma na mikoa mingine.