WLAC yapeleka shuleni, vyuoni elimu ya ukatili wa kijinsia

26Jan 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
WLAC yapeleka shuleni, vyuoni elimu ya ukatili wa kijinsia

KITUO cha Msaada wa Kisheria Tanzania (WLAC), kimeanza mpango wa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika shule za sekondari
na vyuoni.

Mpango huo umelenga kuwasaidia wanafunzi kupambana na vitendo hivyo katika maeneo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Sheria wa WLAC ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni ya kupambana na ukatili wa kijinsia ya Tunaweza inayoendeshwa na kituo hicho, Karilo Mlembe, alisema wameamua kupeleka elimu hiyo kwa sababu shuleni na vyuoni ni maeneo yanayokumbwa na vitendo hivyo kwa wingi mara kwa mara.

Alisema lengo kuu ni kuwaelimisha wanafunzi kufahamu namna tofauti za ukatili huo na jinsi ya kupambana nayo ikiwamo kuhakikisha wanawaripoti katika vyombo husika pale wanapobaini watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Wanafunzi wenyewe wanafanyiwa ukatili kwa namna nyingi mara kwa mara, na tumekuwa tukishuhudia katika vyombo vya habari na hata maeneo mengine namna wanavyofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, wanafanyiwa wakiwa shuleni na wakati mwingine nyumbani, kwa hiyo tunafanya hivyo ili kuwasaidia namna ya kujinasua,” alisema na kuongeza:

“Kwa hiyo wanafunzi, sisi tunalichukulia kama kundi maalum ambalo tumelilenga kulielimisha ili waweze kuona ni namna gani waepukane navyo na pale wanapokuwa katika hali ya ushawishi wajue namna ya kujinasua na hata kufikisha taarifa katika vyombo vya dola na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.”

Alisema katika awamu ya kwanza wamepanga kufikia shule sita za sekondari na vyuo vinne katika mkoa wa Dar es Salaam kutoa elimu hiyo pamoja ikiwamo kuzungumza na wanafunzi ambao wamewahi kukumbwa na tatizo hilo.

Kwa upande wake Mwalimu wa shule ya sekondari ya Makumbusho ambayo WLAC walitoa elimu hiyo, John Shayo alisema wanafunzi wa sekondari bado umri wao ni mdogo ambao wanapaswa kuelimishwa juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ili kuepukana nayo.

Shayo alisema elimu kwa wanafunzi hao itasaidia hata kuwafungua kiakili, kufahamu namna ya kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama pale wanapokutana matukio ya namna hiyo.

Habari Kubwa